CCM yaitaka serikali kukamilisha Sekondari ya Ikungulyambeshi.

Madarasa ya Shule ya Sekondari Ikungulyambeshi yaliyojengwa na Kampuni ya kuchambua Pamba ya Alliance Ginnery iliyoko Kasoli wilayani Bariadi.


NA COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bariadi mkoani Simiyu kimeitaka serikali kukamilisha ujenzi wa shule ya sekondari Ikungulyambeshi ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea kilometa 30 kila siku kwenda Kasoli sekondari.

 

Shule hiyo yenye vyumba vinne vya madarasa imejengwa na Kampuni ya kuchambua Pamba ya Alliance Ginnery kwa thamani ya shilingi Mil. 95.5 ili kuwasogezea huduma ya elimu wanafunzi ambao hutembea mwendo mrefu kila siku.

 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini, Katibu wa CCM wilaya ya Bariadi Masanja Salu amesema Chama Cha Mapinduzi kinampongeza mwekezaji huyo kwa kujitolea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwasogezea huduma wananchi kwenye sekta za elimu, afya na maji.

 

Amesema CCM imetembelea shule ya sekondari Ikungulyambeshi na kukuta yamejengwa madarasa manne na mwekezaji huyo, lakini hakuna nyumba ya mwalimu wala vyoo hali ambayo inakwamisha shule hiyo kuanza kutumika.

 

‘’Niiombe serikali na wadau wengine wakaone shule ile na mazingira iliyopo, pia wawaone wanafunzi wanavyotembea kilometa 15 kwenda na kurudi, jumla kilometa 30…wanafunzi wanahangaika na changamoto za njiani, juhudi za makusudi zinahitajika ili wanafunzi wapate elimu karibu’’ alisema Salu.

 

Dotto Julias mwanafunzi wa Kasoli sekondari alisema kila siku hutembea mwendo wa kilometa 15 asubuhi na jioni kutoka Ikungulyambeshi B kwenda shuleni.

 

‘’Wakati wa masika tunachelewa shule kwa sababu ya ubovu wa barabara,tunatembea umbali wa kilometa 15 kuifuata elimu, tunaiomba serikali ikamilishe vyoo na nyumba ya mwalimu ili tusome karibu…tunaishukuru Allience kwa kutujengea madarasa Ikungulyambeshi Sekondari‘’ amesema Maduka Mashauri, mwanafunzi wa Kasoli sekondari.

 

Meneja wa Alliance Ginnery, Boaz Ogolla amesema kiwanda hicho ni sehemu ya kaya katika kata ya Kasoli, hivyo wana wajibu wa kushirikiana na jamii katika maendeleo yao.

 

Amesema tangu walipoingia mwaka 1998 waliona kuna mapungufu katika jamii inayowazunguka kwenye huduma za afya, elimu na maji hali iliyowalazimu kujiunga nao kuwasaidia kuwasogea huduma za kijamii.

 

‘’Mtazamo wetu ni kuwa na jamii yenye uelewa, wananchi bado wana uhitaji mkubwa wa elimu…juhudi za kujenga shule na miradi mingine wananchi wanatakiwa kuelewa kuwa ni mali yao, hivyo wanatakiwa kuitunza na kuiendeleza’’ amesema Ogolla.

 

Amesisitiza kuwa wataendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuendelea kujenga miundombinu ya kijamii ili kuisaidia serikali kuwasogezea wananchi huduma za kimaendeleo.

 

MWISHO.

 

Madarasa ya Shule ya Sekondari Ikungulyambeshi yaliyojengwa na Kampuni ya kuchambua Pamba ya Alliance Ginnery iliyoko Kasoli wilayani Bariadi.


Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Masanja Salu akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kasoli iliyopo kijiji cha Kilalo mara baada ya kutembelea miradi inayotekelezwa na Kampuni ya Alliance Ginnery katika sekta za Elimu, Afya na Maji.


           Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Masanja Salu.

 


 Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Masanja Salu akiwa na baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kasoli wanaotembea kilometa 30 kila siku kutoka kijiji cha Ikungulyambeshi.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post