Wapendekeza picha Mlima Kilimanjaro kwenye Vazi la Taifa.

 


Na Samwel Mwanga,Maswa.

WAKATI mchakato wa kupata Vazi la Taifa ukiwa unaendelea, wanawake katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wameomba vazi hilo lijumuishe picha za wanyama pori ambao ni hazina ya Taifa.

Sambamba na kuwepo kwa picha hizo pia wamependekeza kuwepo kwa picha ya mlima Kilimanjaro ilikuweza kutambulisha vivutio vikuu ambavyo vinapatikana hapa nchini.

Wakizungumza na Waandishi wa habari mjini baadhi ya wanawake hao wamesema kuwa picha hizo ni muhimu kwa utambulisho wa taifa letu.

Wamesema wakati mchakato huo ukiwa unaendelea huku kamati ya kukusanya maoni ikiendelea na kazi maeneo mbalimbali hapa nchini ni vizuri vivutio hivyo vikaoneka kuliko vitu vingine.

"Tuna mbuga za wanyama hapa nchini ni vizuri vazi la taifa likawa na picha za wanyama wanaopatikana hapa nchini kwanza hata wageni kutoka nje huwa wanakuja kuwaangalia,"alisema Caroline Shayo.


Walisema kuwa nchi yetu huwezi kutaja vivutio vyake bila kuutaja mlima Kilimanjaro ambao ndiyo mlima mrefu barani Afrika.

 "Huwezi kuitaja nchi yetu ya Tanzania bila kivutio cha Mlima Kilimanjaro kwa msingi huo ni vizuri ukaonekana kwenye vazi la taifa letu,"alisema Mwalimu Neema Revocatus.

Antonia Nkolela ambaye ni Katibu wa UWT wilaya ya Maswa alisema kuwa si Wanyama wote wanapaswa kuonekana kwenye vazi hilo bali wale Wanyama wakubwa watano ambao ni Simba,Tembo,Nyati,Kifaru na Twiga.

"Kwa Wanyama sio wote wa kuonekana kwenye vazi la taifa binafsi ningependekeza walao wale Wanyama wakubwa watano ambao ni Simba,Tembo,Nyati,Kifaru na Twiga.

Aidha waliiomba serikali kuharakisha mchakato huo wa kupata vazi hilo ufikie mwisho ili tulipate kwani umeanza muda mrefu lakini bado halijapatikana.

Naye  Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Chifu Antonia  Sangalali  ni miiongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo ambaye amekuwa akihamasisha Wananchi kutoa maoni yao kwa ajili ya upatikanaji wa vazi la Taifa alisema ni vizuri wananchi watoe mawazo yao Kwa uhuru bila ubaguzi wowote kwa kuwa sote hii ni nchi yetu.


Mwisho.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post