DC Simalenga; Pikipiki zitumike kukusanya mapato, kusimamia Ulinzi na Usalama.

MKUU wa Wilaya ya Bariadi Saimoni Simalenga (mwenye suti ya kijivu) akikabidhi funguo za pikipiki kwa mmoja wa Watendaji wa Kata, pikipiki 6 ambazo zimetolewa na TAMISEMI kwa ajili ya kusimamia ukusanyaji wa Mapato, kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Khalid Mbwana akiwa pamoja baadhi madiwani.



MKUU wa Wilaya ya Bariadi Saimoni Simalenga (mwenye suti ya kijivu) akikabidhi funguo za pikipiki kwa mmoja wa Watendaji wa Kata, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Lukas Mayala pamoja na baadhi ya Madiwani.


 MKUU wa Wilaya ya Bariadi Saimoni Simalenga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Madiwani na Watendaji wa kata, mara baada ya kukabidhi pikipiki 6 ambazo zimetolewa na TAMISEMI kwa ajili ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato.


Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

MKUU wa Wilaya ya Bariadi, Mkoani Simiyu Saimoni Simalenga amewataka Watendaji wa Kata kusimamia ukusanyaji wa mapato baada ya serikali kuwapatia usafiri wa pikipiki.

 

Aidha Simalenga amewataka watendaji hao kusimamia ulinzi na usalama wa raia na mali zao ikiwemo kuzuia uhalifu kwa kufanya vikao vya ulinzi na usalama mara kwa mara.

 

Ameyasema hayo leo mara baada ya kukabidhi pikipiki sita zilizotolewa na Ofisi ya Raias-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa Watendaji wa kata kwenye Halmashauri ya wilaya ya Bariadi, zoezi ambalo lilifanyika Dutwa makao makuu ya Halmashauri hiyo.

 

Simalenga amewataka Madiwani kuwasimamia watendaji wa Kata kwenye ukusanyaji wa mapato huku akiitaka Halmashauri hiyo kuongeza mashine za kielektroniki ili kila mtendaji wa kijiji apatiwe mashine yake.

 

‘’Halmashauri hii ina mashine za kielektroniki 69 kati ya vijiji 84, inatakiwa kila kijiji kiwe na mashine yake ili tuweze kukusanya mapato ipasavyo, hivyo Halamshauri tununue mashine zingine ili kila mtendaji apatiwe mashine yake’’ amesema Simalenga.

 

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya amewataka watendaji wa vijiji kufanya vikao vya ulinzi na usalama pamoja na kusoma mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu.

 

Awali akitoa taarifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Mbwana amesema Halamshauri hiyo ilikuwa na mpango wa kununua pikipiki kwa watendaji wa kata zote 21 za Halmashauri hiyo.

 

Amesema zoezi la ununuzi wa pikipiki za Watendaji limefanywa na Wizara ya TAMISEMI kutokana na fedha za kodi ya majengo na kwamba kati ya pikipiki 912, Halmashauri hiyo imepatiwa pikipiki 6.

 

‘’Tumepatiwa pikipiki 6 kati ya 912 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya watendaji wa kata kusimamia ukusanyaji wa mapato, niwaombe watendaji wakasimamie zisigeuzwe bodaboda au usafiri binafsi’’ amesisitiza Mbwana.

 

Nao baadhi ya watendaji wameipongeza serikali kwa kutoa pikipiki hizo huku wakiahidi kuzitumia kulingana na maelekezo yaliyotolewa na serikali.

 

MWISHO.

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post