Wanafunzi wawili wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kasoli wakiwa darasani.
Na Mwandishi Wetu.
CHUO cha Ufundi Stadi (VETA) kilichojengwa na Kampuni ya Ununuzi wa Pamba ya Alliance Ginnery iliyoko Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu kimekosa wanafunzi licha ya kujengwa kwa gharama kubwa na kukabidhiwa serikalini.
Chuo hicho kilichojengwa tangu 2017/18 kimegharimu shilingi milioni 191.6, kiko kijiji cha Busese Kata ya Kasoli chenye majengo matatu yenye vyumba vya madarasa, stoo na ofisi za walimu, vyoo na kina mwalimu mmoja na wanafunzi wawili wanaojifunza kozi ya ushonaji.
Awali chuo hicho kilijengwa kwa lengo la kutoa kozi za Uashi, Ushonaji, Upishi na Uselemala ili kuwarahisishia wananchi kupata ujuzi kina umeme na maji kwa ajili ya kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji.
Joseph Shija, Afisa utumishi Alliance Ginnery amesema mradi huo ulijengwa ili kuwasaidia wananchi wanaozunguka kampuni kupata ujuzi wa fani mbalimbali waweze kulifikia soko la ajira.
‘’Lengo lilikuwa ni kutoa elimu ya ujuzi ili wakajitegemee, hapa kuna fani mbalimbali ikiwemo upishi, ushonaji, ujenzi na uselemara..wanafunzi wakijifunza hapa watapata elimu na hii yote ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia ili nchi iwe na maendeleo’’ amesema Shija.
Ameongeza kuwa Kampuni hiyo iliweka kipaumbele eneo hilo kwa kujenga majengo matatu na vyoo, kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzi pamoja na kuchimba kisima cha maji.
Meneja wa Alliance Ginnery, Boaz Ogolla alisema kiwanda hicho ni sehemu ya kaya katika kata ya Kasoli, hivyo kina wajibu wa kushirikiana na jamii katika maendeleo yao.
Amesema tangu walipoingia mwaka 1998 waliona kuna mapungufu ya kimandeleo katika jamii inayowazunguka katika huduma za afya, elimu na maji hali iliyowalazimu kujiunga kuwasaidia ili kuwasogea huduma za kijamii.
‘’Mtazamo wetu ni kuwa na jamii yenye uelewa, wananchi bado wana uhitaji mkubwa wa elimu…juhudi za kujenga shule na miradi mingine wananchi wanatakiwa kuelewa kuwa ni mali yao, hivyo wanatakiwa kuitunza na kuiendeleza’’ amesema Ogolla.
Amesisitiza kuwa wataendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuendelea kujenga miundombinu ya kijamii ili kuisaidia serikali kuwasogezea wananchi huduma za kimaendeleo.
Ameongeza kuwa walijenga chuo cha VETA ili wanafunzi waliokosa kuendelea na masomo wasibakie kuwa wakulima majumbani na badala yake wapate elimu ya kifundi karibu na maeneo yao bila gharama.
‘’Tulinunua vifaa vya kujifunzia ikiwemo vyerehani, vifaa vya ufundi uashi, upishi na userelama sababu hizi fani zinahitajika katika jamii…chuo hakijafanya vizuri sana, tunaiomba serikali kuweka mkono wake pale ili wanafunzi wapate ujuzi’’ amesema Ogolla.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Masanja Salu amesema VETA hiyo imejengwa ili vijana wanaokosa kuendelea na masomo ya sekondari na vyuo vikuu waweze kupata elimu ya ujuzi bila ada yoyote.
Amewataka wazazi na walezi kupeleka vijana katika chuo hicho ili wakapate elimu ya ujuzi na maarifa na waweze kujiajiri kupitia fani mbalimbali ambazo zitawarahisishia maisha.
MWISHO.
Cherehani inayotumia umeme ikiwa katika darasa la Ushonaji, chuo cha ufundi stadi (VETA) Kasoli.
Vyoo vya chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Kasoli.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment