Kiwanda Bubu cha Kutengeneza Konyagi chakamatwa Bariadi.


 

 Nyumba iliyokuwa inatumika kama Kiwanda Bubu kwa ajili ya kutengeza Pombe kali aina ya Konyagi iliyoko mtaa wa barabara ya Stephano, Mtaa wa Budeka, Kata ya Sima katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

 

 

 

 Mtambo au ndoo aina ya Diaba iliyokuwa inatumika kuchanganya Spriti na Maji kienyeji ili kupata Pombe kali aina ya Konyagi katika mtaa wa Budeka, kata ya Sima, Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

 

 

 

 Baadhi ya Maboksi yakiwa yamefungashiwa chupa za Pombe kali aina ya Konyagi ambayo ilikuwa inatengenezwa kienyeji katika Mtaa wa Budeka, Kata ya Sima kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

 

Vijana wawili ambao hawakufahamika majina mara moja wakiwa wamekatwa na kuwekwa kwenye gari la Polisi pamoja na bidhaa feki ya Konyagi kwa ajili ya kupelekwa kituo cha Polisi mjini Bariadi.

 

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

KAMATI ya Ulinzi na Usalama wilaya ya Bariadi imekamata kiwanda Bubu kilichokuwa kikitengeneza Pombe kali aina ya Konyagi katika mtaa wa Budeka, Kata ya Sima kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi.

 

Katika uchunguzi uliofanywa na waandishi wa Habari waliofika eneo la tukio, umebaini bidhaa hiyo ilikuwa ikizalishwa kienyeji licha ya kuwa na nembo halali ya Konyagi, stika za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini pia bidhaa hiyo haina tarehe ya kuanza kutumika wala tarehe ya mwisho wa matumizi (Expire date).

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wilaya ya Bariadi Nichodemus Shirima amesema wamekamata watu wawili waliokuwa katika kiwanda hicho bubu na kwamba tukio la kuwa na kiwanda Bubu cha kutengeneza Konyagi ni baya sana kutokana na madhara wanayoyapata watumiaji.

 

‘’Hiki kinywaji hakijapimwa, hakina TBS, hakuna mtu anayejua kama kinywaji hiki ni sumu au laah…inaonekana kuna ulegevu katika ukaguzi mpaka watu wameamua kuanzisha viwanda bubu katika makazi ya watu lakini tunashukuru hatimaye wamebainika’’ amesema na kuongeza.

 

‘’Tunaiagiza Mamlaka ya serikali za mitaa, wawe na takwimu za wakazi kwa kila mtaa ili kuwatambua wakazi waa eneo lile kwa nyumba, namba zao na picha na ibainike shughuli wanawazofanya na wale ambao hawataki kufungua mageti waende polisi kutoa taarifa ili kubaini shughuli wanazofanya’’

 

Shirima amesema suala hilo haliwezi kuvumiliwa huku akiahidi kuongeza ufuatiliaji ili kuhakikisha wanadhibiti vitendo vya kihalifu vinavyofanyika ambapo serikali inapoteza mapato huku wananchi wakipata madhara kiafya kutokana na kuuziwa bidhaa feki ikiwemo Konyagi.

 

Amesema wamebaini mazingira ya eneo hilo siyo salama lakini usalama wa maji yanayotumika kuchanganyia Konyagi hiyo hayana usalama huku akiwaonya wengine wanafanya vitendo hivyo kuacha mara moja.

 

Amewataka wafanyabiashara na wananchi ambao wameshanunua bidhaa hiyo feki ya Konyagi, kuisalimisha mara moja kwenye ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi au kituo cha polisi ili wasichukuliwe hatua za kisheria endapo watabainika.

 

Kwa upande wake Ofisa Tarafa ya Ntuzu Rashid Zongo amesema bidhaa hiyo imeleta madhara makubwa mtaani, lakini hawawezi kupata viwango halisi ambavyo Konyagi wanavitengeneza na watumiaji walionunua konyagi hiyo kutoka kiwanda bubu wanaweza kupata madhara.

 

‘’wanahujumu uchumi, serikali haipati mapato kwa sababu wamejificha na hawana leseni, wanaiba na tutawafuatilia popote walipo na kama waaendelea tutawakamata…tulipata taarufa toka kwa wasamalia wema na kufanikiwa kuwakamata’’ amesema Zongo.

 

Mwenyekiti wa mtaa wa Budeka Leonard Mahande Mayunga amesema alipata taarifa kutoka kwa maaskari polisi kuwa kuna kiwanda bubu cha kutengeneza Konyagi katika mtaa wake jambo ambalo hata yeye lilimshangaza.

 

Anasema baada ya taarifa hiyo, alimpigia simu mjumbe wa serikali ya mtaa ili awahi eneo hilo na baada ya yeye kufika eneo hilo alikuta nyumba hiyo ikiwa inatumika kama kiwanda bubu cha kutengeneza pombe aina ya Konyagi.

 

Amesema mpangaji huyo aliletwa na madalali kwa madai kuwa anahitaji kupangishwa nyumba nzima kwa ajili ya makazi na wakati wa kusainishana mkataba alieleza kuwa ni mkazi wa Mkoa wa Mwanza

 

Majirani wanena.

 

Jonh Malimi mkazi wa mtaa wa Budeka ambaye ni jirani na nyumba hiyo, amesema aliitwa na maaskari polisi kwa ajili ya kushuhudia upekuzi wa nyumba iliyodhaniwa kutengeneza bidhaa feki ya Konyangi.

 

Anasema alifika eneo la tukio na kukuta uzalishaji ukiendelea ambapo aliona mapipa mawili ya spriti, diaba moja lenye koki linalotumika kumiminia konyagi, maboksi ya konyagi ndogo zaidi ya 39 ambayo yameshafungashwa kwa ajili ya kupelekwa sokoni.

 

Salu Mbiragana mjumbe na mkazi wa Mtaa wa Budeka amesema amekuta hali hiyo kwenye nyumba hiyo mtaa wa Stephano baada ya kupigiwa simu na Mwenyekiti wa Mtaa ili ashuhudie kinachofanyika humo.

 

‘’Nimekuta mapipa mawili na Spriti, chupa tupu na maboksi ambayo yamewekewa pombe hizo na nilikuta juu ya meza kuna diaba lenye spriti kwa ajili kujaza pombe kwenye chupa, niliona pia stika zenye nembo za Konyagi na zingine zimeshatumika, nimeona kwenye nyumba hii kuna vijana walikuwa wanaishi’’ amesema Mbiragana.

 

Amesema matukio hayo yanazua taharuki katika mitaa na pia ni kero kwa jamii na matukio hayo yamekithiri huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea na ukaguzi kwa kila nyumba ili kubaini wahalifu na uhalifu.

 

MWISHO.

 

 

 

 

Baadhi ya maboksi ya Konyagi ambayo hayajatumika.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post