MWENYEKITI wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi David Masanja (aliyesimama) akizungumza wakati wa kufungua kikao cha Baraza la Madiwani, kulia ni Makamu Mwenyekiti Kija Bulenya, kushoto ni Mbunge wa Vijana Mkoa wa Simiyu Lucy Sabu pamoja na Kaimu Mkurugenzi Maganiko Barnbas.
Katibu Tawala wilaya ya Bariadi Nichodemus Shirima akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika ukumbi wa Bariadi Sekondari.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MADIWANI wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu wamewataka Vijana, Wanawake na Walemavu kuhakikisha wanazingatia masharti wanayopewa na serikali kuhusu mikopo ya asilimi 10 ili waendelee kuaminika na kukopesheka.
Hayo yamebainishwa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, David Masanja kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika katika ukumbi wa Bariadi Sekondari kwa ajili ya kujadili taarifa za robo ya pili.
Alisema lengo la serikali kutoa mikopo hiyo ni kuwaimairisha kiuchumi, kuwajengea uwezo wa kujiongezea kipato ambapo kupitia mikopo hiyo inayotolewa na serikali bila riba kwa Vijana, Wanawake na Walemavu baadhi yao wameanza kunufaika.
Masanja aliwataka Vijana, Wanawake na Walemavu kuendelea kutumia elimu wanayopewa na serikali juu ya utaratibu wa kurejesha mikopo isiyokuwa na riba ili na watu wengine wanufaike.
‘’Tunaendelea kuwaomba Vijana, Wanawake na Walemavu kuhakikisha wanarejesha mikopo waliyopewa na serikali ili wengine waweze kunufaika, baadhi ya maeneo wameshapelekwa mahakamani, lakini hapa kwetu tunaendelea kuwasimamia kwa kushirikiana na wataalamu wa Halmashauri’’ alisema Masanja.
Alisema haitapendeza kama vijana, wanawake na walemavu wakakosa sifa ya kupata mikopo licha ya kukidhi vigezo kutokana na wengine kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo aliitaka serikali kuondoa masharti kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu ili kila kikundi chenye sifa kiweze kukopesheka hata kama wanahitaji fedha kidogo.
Awali akizungumza kwa niaba ya Serikali, Katibu Tawala wa Wilaya ya Bariadi, Nichodemus Shirima aliiomba halmashauri hiyo kuendelea kutoa elimu na kuwasimamia vijana, wanawake na walemavu ili waweze kurejesha mikopo hiyo.
Alisema, serikali haitakubali kuendelea kutoa mikopo kwa vijana, wanawake na walemavu wakati huo baadhi ya vikundi vinashindwa kurejesha mikopo hiyo.
‘’Tuendelee kuwasimamia vijana, wanawake na walemavu ili tufikie malengo ya serikali kutoa mikopo ya asilimia 4 (vijana), 4 (wanawake) na 2 (walemavu)…tuvisimamie vikundi hivyo ili virejeshe mikopo kwa wakati na watu wengine waweze kunufaika’’ alisema Shirima.
Sambamba na mambo mengine, kikao hicho pia kilijadili taarifa za maendeleo ya kata pamoja na taarifa za kamati mbalimbali za kudumua za Halmashauri hiyo.
MWISHO.
Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika ukumbi wa Bariadi Sekondari.
إرسال تعليق