Matukio ya mauaji Simiyu yameanza kurejea tena.

 


Na Mwandishi wetu, Simiyu.


Matukio ya mauji ya watu mbalimbali hasa watoto, wazee, na wanawake yakitajwa kusababishwa na imani za kishirikiana, migogoro ya kifamilia katika Mkoa wa Simiyu yanadaiwa kurejea tena.


Miaka mitano nyuma matukio haya yalikomeshwa kwa kiwango kikubwa. Sasa yanatajwa kuanza kurejea upya kutokana na taarifa za kila siku kuonyesha lazima kuwepo kwa tukio mtu kuuawa.


Kabla ya kukomeshwa, Mkoa wa Simiyu ulisifika kwa matukio hayo, ambapo waganga wa tiba asili walitajwa kuwa kichocheo kikubwa cha uwepo wa matukio hayo kwa wingi.


Kuanzia wiki iliyopita viongozi wa Mkoa huo kwa nyakati tofauti tofauti likiwemo Jeshi la Polisi, wamezumgumzia kurejea kwa matukio hayo.


RC.


Mkuu wa Mkoa Dkt. Yahya Nawanda akiwa kwenye hafla ya kukabidhi zawadi Askari waliofanya vizuri mwaka 2012, iliyofanyika Februari 04, 2023 (jumamosi ya wiki iliyopita) alizumgumzia matukio hayo.


Kwa mujibu wa Dkt. Nawanda kwenye Hafla hiyo ambayo alikuwa mgeni rasmi, alisema kuwa kila siku amekuwa akipewa taarifa na Kamanda wa Polisi Mkoani humo uwepo wa matukio mauaji.


Dkt. Nawanda amesema kuwa matukio ya mtu kuuawa kwa imani za kishirikina au migogoro ya kifamilia, yameanza kuongezeka kwani kila siku lazima kuwepo kwa tukio.


Anasema kuwa matukio yanayosababishwa na imani za kishirikina ndiyo yamekuwa mengi, yakifuatiwa na migogoro ya kifamilia, pamoja na ukataji wa mapanga, ambapo wazee, wanawake na watoto ndiyo waanga.


“ Kila siku RPC akinipigia simu utasikia anakwambia leo kuna mtu mmoja ameuawa, siku nyingine akisema hakuna tukio unamshukuru Mungu, lakini haya matukio sasa yameongezeka, yamekuwa mengi,” anasema Dkt. Nawanda….


“ Hizi tabia tumezitoa wapi sisi wasukuma, mbona sisi siyo watu wa hivi, hizi tabia mbona zilipotea, sasa zinatoka wapi?” anasema Dkt. Nawanda.


Mkuu huyo wa Mkoa anawataka wagaga wa tiba asili kuanzisha kampeini ya kupita vita kurejea kwa matukio hayo, huku akilitaka jeshi la kupambana na hali hiyo.


DC.


Siyo tu Mkuu wa Mkoa ambaye amezungumzia kuanza kurejea kwa matukio ya mauji mkoani hapa.


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Simon Simalenga akizungumza na waandishi wa Habari jana, amesema kuwa ndani ya wiki moja jumla ya watu watano wameuawa, wakiwemo watoto, wazee na wanawake.


“ Uko nyuma haya mauji yalikomeshwa kabisa, lakini tumeona yanataka kuanza kurudi, ndani ya wiki moja watu watano wameuawa, wapo watoto, wazee na wanawake, na yote yanahusishwa na imani za kishirikina ikiwemo migogoro ya kifamilia,” Amesema Simalenga.


Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa akiwa kama Mkuu wa Wilaya hiyo, atahakikisha matukio hayo yanakomeshwa huku akitumia msemo kuwa “ Afe kipa, afe Beki, lazima mauji Bariadi yakomeshwe,” amesema Simalenga.


RPC.


Kamanda wa Polisi mkoani hapa Blasius Chatanda kwenye hafla ya kutoa zawadi kwa Askari, anakiri matukio ya mauji kuanza kuongeza ambapo anasema wameanza kupambana nayo.


Chatanda anasema wanawashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo waganga tiba asili katika kupambana na matukio hayo ili kuweza kukomeshwa kabisa.


MWISHO.



Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post