Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MAMIA ya Waombolezaji kutoka Wilaya ya Bariadi na Mikoa jirani ya Shinyanga, Mwanza na Geita wamejitokeza kwenye mazishi ya aliyewahi kuwa Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Bariadi Masuke Tunge kutoka mwaka 1971 hadi 1975.
Akiongoza mazishi hayo, Mkuu wa wilaya ya Bariadi Simon Simalenga amesema maisha ya watu duniani ni mafupi sana, hivyo kila mmoja anatakiwa kujiandaa na safari ya mwisho ya hapa duniani.
‘’hakuna atakayekumbukwa kwa uzuri wa jeneza au kaburi kupambwa…hivyo kila mmoja atakumbukwa kwa mazuri aliyotenda, tutende mema na tuache alama kwa watu tunaoishi nao’’ amesema Simalenga.
Akitoa salamu za Chama Cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo amewataka kila mmoja kufanya maandalizi juu ya safari ya maisha yake huku akisisitiza kutowabeza viongozi wa dini.
Amesema alimjua Masuke tangu mwaka 1970 wakati akiwania Ubunge pamoja na mme wake (Edward Ng’wani) kupitia Chama cha Mapinduzi wakati wilaya ikiwa bado ni moja ya Maswa.
‘’Nilienda kushuhudia uchaguzi huo wa mme wangu na Masuke, hakuna jambo la aibu kama kushindwa…kwenye kura tulienda pamoja lakini tuliposhindwa niliondoka pekee yangu, tutafakari neno la Mungu ili tuwe watu wa kushinda kwenda mbinguni’’ amesema Mwenyekiti huyo.
Ameongeza kuwa Marehemu Masuke amekuwa mtumishi wakati wa chama kimoja cha TANU mwaka 1970 na mwaka 1975 alishindwa ubunge na Edward Ngh’wani.
Awali akisoma wasifu wa Marehemu, Isack Ngasani ambaye ni Mjukuu wa Marehemu amesema Masuke Tunge alizaliwa Januari 9, 1933 katika kijiji cha Sanungu, wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu akiwa ni mtoto wa tano kati ya watotot tisa wa Mzee Tunge Ipilinga.
Amesema Marehemu hakubahatika kupata elimu katika mfumo rasmi, isipokuwa alijifunza kusoma na kuandika kutoka kwa mwalimu Deusi na baada ya kuingia kwenye siasa alisoma kwa njia ya posta na alihitimu darasa la nne 1967 nchini Kenya.
‘’Alijiunga na Chama cha TANU, October 28, 1958 na baadae kujiunga na TANU YOUTH LEAGUE kama askari wa TANU mwaka 1958, alikuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya wilaya ya Maswa kwa tiketi ya vijana kutoka Ntuzu chiefdom 1959’’ amesema na kuongeza.
‘’Alikuwa Diwani wa Council ya Subchiefdom ya Ntuzu mwaka 1961, mwaka 1962 akachaguliwa kuwa diwani wa kata ya Somanda, pia akawa Katibu wa TANU tawi la Mhango (TANU Collector)…mwaka 1964 alikuwa mwenyekiti wa Council ya Maswa hadi mwaka 1970’’.
Amefafanua kuwa mwaka 1969 hadi 1972 alikuwa Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shinyanga Cooperative Unioni (CUT), pia aliwahi kuwa Mbunge wa Wilaya ya Bariadi mwaka 1971 hadi 1975.
Amesema mwaka 1972 alikuwa mjumbe wa Taifa wa TAPA (Tanganyika African Parents Association), mwaka 1976 hadi 1980 alikuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Nyanza Cooperative Unioni.
Pia mwaka 1983 hadi 1985 alikuwa Katibu Tarafa ya Kishapu, mwaka 1985 hadi 1989 alikuwa katibu Tarafa ya Kanadi hadi alipostaafu utumishi wa Umma mwaka 1989, pia mwaka 1990 hadi 1995 alikuwa Mwenyekiti wa CCM kata ya Somanda.
Marehemu Masuke Tunge ameacha wajane wawili, watoto 19, wajukuu 57 na vitukuu 34, Bwana Alitoa na Bwana Ametwaaa…Jina lke lihimidiwe. AMINA.
MWISHO.
Viongozi wa dini kutoka Kanisa la AICT wakiongoza Ibaada ya kuaga mwili wa Marehemu Masuke Tunge aliyewahi kuwa Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Bariadi tangu mwaka 1971 hadi 1975 kwa tiketi ya CCM.
Masuke Tunge aliyewahi kuwa Mbunge wa kwanza wa Jimbo la Bariadi kutoka CCM mwaka 1971 hadi 1975.
Wajukuu wa Marehemu Masuke Tunge wakiwa wamebeba jeneza.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Juliana Mahongo akionyesha picha ya Marehemu Masuke Tunge enzi za ujana wake wakati anagombea Ubunge Jimbo la Bariadi mwa 1971, alimshinda Edward Ng'hwani (Mme wa Juliana Mahongo).
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق