Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa,Enos Missana akizungumza kwenye maazimisho Wiki ya Sheria mwaka 2023. |
Na Samwel
Mwanga,Maswa.
HAKIMU Mkazi Mfawidhi
wa Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Enos Missana ametoa wito kwa
jamii kuwasaidia misaada mbalimbali Wazuiliwa 74 ambao ni raia wa
Ethiopia walioko katika Gereza la Malya lililoko wilayani humo.
Akizungumza katika
kilele cha Wiki ya Sheria kilichofanyika kwenye Viwanja vya Mahakama ya Wilaya,
amesema kuwa Wazuiliwa hao ambao si Mahabusu wala Wafungwa wapo katika Gereza
hilo kwa kipindi cha miaka Minne tangu kumaliza adhabu yao.
Hakimu Misana ameeleza
mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge ambaye alikuwa mgeni rasmi
katika sherehe hizo kuwa Wazuiliwa hao wana hali mbaya inayotia huruma kutokana
na kutokupata mahitaji yao muhimu kama vile Viatu,Mavazi,Sabuni,Mishwaki na
dawa za meno.
Amesema kuwa Wazuiliwa
hao hawana ndugu ambao wamekuwa wakiwatembelea kama ilivyo kwa mahabusu na
Wafungwa wengine walioko kwenye Gereza hilo.
"Hawa Wazuiliwa
hawana ndugu kama ilivyo kwa mahabusu na Wafungwa walioko kwenye gereza hilo
hivyo yale mahitaji ya msingi wanashindwa kuyapata kweli Wana hali ngumu,"
"Na kwa sasa
wamekuwa wakisaidiwa na Mkuu wa Gereza hilo na wakati mwingine na wafungwa na
mahabusu walioko ndani ya gereza hilo watu hao wanahitaji
kusaidiwa,"amesema.
Hakimu Missana amezidi
kuelezea kuwa wakati wa Wiki ya Sheria mara baada ya kutembea gereza hilo na
kutoa Elimu ya sheria pia katika ukaguzi wa Magereza kama yaliyo majukumu yake
ya kawaida ndipo alipobaini kuwepo Kwa Wazuiliwa hao ambao kesi zao za Uhamiaji
zilishakwisha hivyo wanasubiri Serikali ya nchi yao kuwasafirisha kuwarejesha
nchini Ethiopia.
Amesema wao wakiwa
watumishi wa Mahakama katika wilaya hiyo na Wadau wengine waliweza
kuchangishana vitu mbalimbali kwani kwa mwaka huu wameanzisha kitu
kipya kiitwacho"Tendo la huruma kwa Wenye Uhitaji" na
hivyo kuomba watu wengine walioguswa waweze kuwasaidia kwani hao ni binadamu
wenzetu licha ya kutokuwa ni Raia wa nchi yetu.
"Kwa taratibu
zinavyoonekana hawa Wazuiliwa bado wataendelea kukaa kwenye gereza hilo hivyo
niwaombe watu wengine walioguswa waweze kuwasaidia watu hao,"amesema.
Mkuu wa wilaya ya
Maswa,Aswege Kaminyoge ameuomba Uongozi wa Uhamiaji mkoa wa Simiyu waweze
kuharakisha taratibu zinazotakiwa ili raia hao wa Ethiopia waweze kurejeshwa
katika nchi yao.
Pia amemwagiza Katibu
Tawala Wa Wilaya hiyo,Agnes Alex kuandaa utaratibu Ili waweze kufika katika
gereza la Malya na kuwaona hao Wazuiliwa.
"Niombe Uongozi
wa Uhamiaji mkoa wa Simiyu uweze kuharakisha Ili kuhakikisha raia hao wa
Ethiopia waliozuiwa katika gereza la Malya wanaweza kurejeshwa kwao pia Katibu
Tawala Wa Wilaya andaa utaratibu tukawaone kama walivyofanya watumishi wa
Mahakama,"amesema.
MWISHO.
إرسال تعليق