Wananchi wa Kijiji Cha Mwashegeshi wilaya ya Maswa waliohudhuria katika hafla ya Mauwasa ya kumkabidhi mkandarasi,Bal BUILDERS LTM kutekeleza Mradi wa Maji katika Kijiji hicho. |
Na Samwel Mwanga,Maswa.
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira
mjini Maswa (Mauwasa) iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu inatekeleza
Mradi wa Maji safi ya Bomba katika Kijiji Cha Mwashegeshi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Mauwasa aliyewakilishwa na Leonard Mnyeti wakati wa hafla ya
kumtambulisha Mkandarasi BAL BUILDERS LTM ambaye ndiye atatekeleza mradi
huo,kwa wananchi wa kijiji hicho.
Akitoa taarifa kwa wananchi juu ya
Mradi huo Mnyeti alisema kuwa utagharimu kiasi cha sh milioni 500.7 na
Mkandarasi huyo atafanya kazi chini ya Usimamizi wa Mamlaka hiyo.
"Mradi huu wa maji utagharimu
kiasi cha sh 530,752,361.50 na huyu mkandarasi ambaye tunamtambulisha kwenu
atafanya kazi chini ya uangalizi wetu sisi Mauwasa na si
vinginevyo,"alisema.
Alisema kuwa kijiji hicho licha ya
kupakana na bwawa la New Sola ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji
wa Maswa na vijiji 11 lakini walikuwa si wanafaika wa maji hayo.
Alisema mtandao wa maji katika mradi
huo utakapokamilika utakuwa wa kilomita 14.3 na utakamilika ndani ya kipindi
Cha miezi tisa.
"Tunategemea ndani ya miezi tisa
mradi utakuwa umekamilika na mkandarasi atatukabidhi na mtaanza kupata maji
safi na salama na mtandao wetu wa Maji utakuwa wa kilomita 14.3 hivyo niwaombe
wananchi mpatieni mkandarasi ushirikiano Ili mradi umalizike kwa
wakati,"alisema.
Aidha aliomba uongozi wa Kijiji hicho
kuhakikisha kuwa wale baadhi ya wafugaji wanaoingiza mifugo yao kwenye bwawa
hilo wanawazuia kwani wakiachiwa watasababisha kukauka Kwa bwawa hilo kwa
kuingiza kiasi kikubwa cha tope.
Diwani wa Kata ya Nguliguli,Peter
Mlyandengu Mathias ameipongeza serikali kwa kutoa fedha ambazo zitatekeleza
mradi huo ambapo ametoa rai kwa wananchi kulinda miundombinu itakayowekwa ya
maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Alisema kuwa kijiji hicho lilikuwa na
shida ya maji safi na salama licha ya kuwa walinzi wa bwawa la New Sola hivyo
Mradi huo utakapokamilika Ile adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta Maji
watautumia kufanya shughuli za uzalishaji mali.
Pia alisema kuwa wako tayari
kumpatia ushirikiano mkandarasi huyo huku akisisitiza wananchi wa kijiji hicho
hasa vijana kupatiwa kazi katika mradi huo ambazo ziko ndani ya uwezo wao.
MWISHO.
إرسال تعليق