Jengo la Zahanati katika Mtaa wa Nyangaka, Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Baadhi ya wakinamama wakiwa kwenye jengo la Zahanati katika mtaa wa Nyangaka, jengo ambalo limejengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Taifa wa TASAF, Peter Ilomo (kulia) akikagua ujenzi za zahanati ya Nyangaka, katikati ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi Saimon Simalenga, na kushoto ni Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bariadi Masanja Salu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WANANCHI wa Mtaa wa Nyangaka katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wameipongeza Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kuwajengea zahanati, jambo ambalo litawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma ya matibabu nje ya Mtaa huo.
Zahanati hiyo ambayo imejengwa na kugharimu shilingi milioni 92, imejengwa kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF kwa ajili ya kuwasogezea wananchi huduma za kijamii.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kamati ya Uongozi wa Taifa wa TASAF, kufika eneo hilo kwa ajili ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi, baaadhi ya wananchi walisema awali walilazimika kutembea kwenda kituo cha afya Muungano na hospitali ya halmashauri ya mji Bariadi -Somanda ili kupata huduma ya matibabu.
Johnson Mgeta mkazi wa Mtaa wa Nyangaka aliipongeza serikali kwa ujenzi wa zahanati hiyo ambayo itawapunguzia adha ya kutembea mwendo mrefu na kwamba itakuwa mkombozi wa afya za wakinamama wajawazito na watoto wachanga.
Naye Silu Nilla alisema kabla ya ujenzi wa zahanati hiyo walikuwa wanafuata huduma ya matibabu kituo cha afya Muungano na Hospitali ya Somanda a,mbapo kwa sasa watapata huduma jirani na makazi yao.
''Tunaishukuru serikali kupitia TASAF kwa kutujengea zahanati katika mtaa wetu, tutaanza kupata huduma jirani na makazi yetu...tunaiomba serikali iharakishe kutuletea watumishi pamoja na madawa ili huduma zianze kutolewa kwa wakati'' alisema Silu.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Nyangaka, Mahenda Mayaya alisema mtaa huo una wakazi 3220 ambao watanufaika zahanati hiyo pamoja na wananchi wengine wa mitaa jirani.
Alisema kwamba baada ya Zahabati hiyo kukamilika itagaharimu zaidi ya shilingi milioni 92.4 fedha ambayo imetolewa kupitia mradi wa TASAF ili kuwasogezea wananchi huduma za kimatibabu jirani na makazi yao.
Kwa Upande wake Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Grace Magembe aliyekuwa ameongozana na Kamati ya Uongozi ya TASAF alimwagiza Mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakikisha kuwa wanaiingiza zahanati hiyo kwenye mipango ya halmashauri ya mwaka 2023/2024.
Alimtaka kuhakikisha wanakamilisha kichomeo taka pamoja na kuleta vifaa tiba na madaktari ili zahanati hiyo ianze kufanya kazi ya kuhudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Taifa wa TASAF, Peter Ilomo aliwataka wananchi wa Nyangaka kuitunza miundombinu ya zahanati hiyo na kwamba waingize maombi ya ujenzi wa nyumba ya Mganga wa zahanati hiyo kwenye mpango kwaajili ya utekelezaji wa bajeti ya mwezi julai mwaka huu.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق