Na Bahati Sonda, Simiyu.
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano waTanzania Kasimu Majaliwa ameagiza stendi kuu ya mabasi - Somanda iliyopo katika mji wa Bariadi Mkoani Simiyu ianze kutumika kwa mabasi makubwa na madogo ili kuondoa usumbufu kwa abiria.
Aidha ameutaka uongozi wa Mkoa kuhakikisha unaweka utaratibu utakaofaa ili mabasi kuwa yanaanzia kwenye stendi hiyo na kuishia hapo lakini si kwa lengo la kuwapitiliza abiria wanaoshukia au kupandia njiani.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo mapema jana wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Mji wa Bariadi akiwa njiani kuelekea Maswa.
“Nilifanikiwa kuitembelea ile stendi kuu na kuona kuwa fedha za Serikali zinapotea bure kwa sababu, kuna vibanda 148 vya wajasiriamali lakini hawafanyi kazi kutokana na kukosekana kwa abiria wanaoingia na kutoka. "Lakini pia niliwaona vijana wa bajaji na bodaboda wamejipanga vizuri isipokuwa hawana kazi kwa sababu hakuna mabasi,” Amesema
Amesema kuwa Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 7 ili zitumike kuupanga mji wa Bariadi na pia ikaanzisha mfumo wa anuani za makazi ili uwepo urahisi wa kufikika hivyo wakati umefika wa kujipanga vizuri ili mji uweze kupangika kwani ndiyo makao makuu ya mkoa.
Katika hatua nyingine amezungumzia suala la eneo la kupaki malori na kusema kuwa kuwepo kwa malori katika eneo hilo kutafungua ajira kwa vijana mafundi wa magari, mafundi umeme, wauza vipuri na mafundi gereji.
"Malori hayatakiwi kupaki hapa mjini kiholela badala yake yaende kwenye eneo lake lililotengwa, yote yaende kule na halmashauri hakikisheni mnaboresha eneo lile kwa kuweka huduma zote za msingi" Amesisitiza Majaliwa
Sambamba na hayo Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mkoa kuacha tabia ya kuwabana wajasiriamali badala yake wawaelimishe na kuwapa miongozo ili wajiendeleze kiuchumi.
MWISHO.
إرسال تعليق