Na Bahati Sonda, Simiyu.
Hatimaye Biashara ya magari madogo ya kubeba abiria (Mchomoko) katika Mkoa wa Simiyu, imerejeshwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa baada ya kuondoa zuio lililoweka na uongozi wa mkoa mwaka jana.
Julai 13, 2022 aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa huo David Kafulila aliweka zuio la magari hayo kufanya kazi ya kusafirisha abiria ndani ya mkoa huo, hiyo ni baada ya kutokea ajali mbili mfulululizo na kusababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 17 ndani ya siku 12.
Hata hivyo tangu kuwekwa kwa zuio hilo, viongozi mbalimbali wa kiasiasa mkoani humo, kikiwemo Chama cha Mapinduzi, wamekuwa wakilalamikia uhamuzi huo na kutaka zuio hilo kuondolewa kwa maelezo kuwa umewafanya vijana wengi kubaki bila kazi.
Mbele ya wananchi, Waziri Mkuu amefuta zuio hilo, na kutaka magari hayo yafanye biashara kama kawaida, lakini yafuate sheria zote za usalama Barabarani, huku pia akielekeza kusajiliwa.
Amesema kuwa Magari hayo yaendelee na shughuli zake za kusafirisha abiria kama kawaida kwa kuzingatia miongozo ya kisheria, kanuni na taratibu za nchi.
"Hatuzuii kufanya shughuli zenu za kusafirisha abiria lakini hakikisheni mnafuata sheria, beba abiria peleka popote, hatuzuii mark 11,Carina probox, kufanya biashara lakini zingatieni sheria kama gari ina viti vitano basi abiria wawe watano, wafunge mikanda, RPC unanisikia na kamanda wa Usalama Barabarani
Aidha Waziri mkuu ametangaza utaratibu mpya wa magari hayo kufanya kazi, kuwa yatasajiliwa rasmi kufanya shughuli hizo, ambapo ameelekeza utaratibu huo ufanyike katika mikoa yote nchi nzima ambayo magari hayo yanafanya kazi.
"Hatukuzuii kuwa mjasiliamali kwenye gari lako kama umefuata taratibu na sheria za nchi na isipokuwa tunataka tuone bodaboda, bajaji, magari madogo na makubwa yakifanya kazi ili muweze kupata vipato vitakavyokidhi mahitaji yenu"Amesema Waziri Mkuu.
Aidha amewataka viongozi wa Mkoa huo, kuacha utaratibu wa kufungua au kuzuia biashara za wajaslimali ambao wanajipatia kipato kwa njia halali, na badala yake akawataka kutumia nafasi hiyo kuwaelimisha na kuwaelekeza.
"Najua Mkuu wa Mkoa aliweka zuio la magari haya, ni mamlaka yake, sasa rasmi leo tumefungua milango magari haya yaanze kufanya kazi, kikubwa wekeni utaratibu ambao unazingatia sheria zote za usalama Barabarani," alisema Waziri Mkuu.
MWISHO.
إرسال تعليق