Wamiliki wa vibanda kwenye masoko Simiyu ni Viongozi

Muonekano wa Soko la Bariadi, Mkoani Simiyu kwa ndani.

Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu Aron Missanga akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya miezi mitatu ya shughuli zinazotekelezwa na taasisi hiyo.

 

Na Derick Milton, Simiyu.


Taasisi ya kuzuia na kupamba na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Simiyu imesema kuwa vibanda vingi kwenye masoko ya Halmashauri za Wilaya ya Maswa, Meatu na Bariadi vinamilikiwa na viongozi.


Aidha taasisi hiyo imesema kuwa baadhi ya viongozi wanamiliki vibanda zaidi ya kimoja kwenye masoko hayo na kuvitumia kwa kujinufaisha wenyewe tofauti na malengo ya serikali ya kuwasaidia wafanyabishara wadogo na wale wa kati.


Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo kwa miezi mitatu kwa waandishi wa habari leo Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa Aron Missanga, amesema kuwa uchunguzi walioufanya umebaini kuwa viongozi hao walitumia madaraka yao vibaya kwa kuhodhi vibanda hivyo.


“ Tulichobaini ni kuwa baadhi ya viongozi ndiyo wamiliki wa vibanda hivyo, tena wanamiliki vibanda viwili hadi vitatu, kisha wanawapangisha wafanyabishara kwa bei kubwa, na wanalipa kiasi kidogo kwenye halmashauri huku wakichukua kiasi kikubwa kwa wafanyabishara”….


“ Lengo la serikali kujenga masoko haya ni kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na wao wapate sehemu za kufanyabiashara wajipatie kipato kwa gharama nafuu, lakini hilo haliko hivyo kwenye masoko yetu, vibanda vingi vimehodhiwa na viongozi,” amesema Missanga.


Naibu Mkuu huyo wa Takukuru amesema kuwa katika uchunguzi wa mfumo wa upangishaji wa masoko hayo, baada ya kubaini jambo hilo waliwaita wamiliki wa soko ambao ni halmashauri kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi.


Amesema kuwa baada ya kuwaita wamiliki, walikaa kikao na kufanya mazungumzo kisha kuweka maazimio, ambayo ameeleza Halmashauri wametakiwa kwenda kuyafanyia kazi kadri walivyokubaliana.


Katika hatua nyingine taasisi hiyo imesema kuwa ndani ya pindi hicho jumla ya kesi 8 ambazo ilizifikisha mahakamani na kutolewa uhamuzi, kati ya hizo 7 takukuru ilishinda huku ikishindwa kesi moja.


Taasisi hiyo imesema kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa ambayo imepata, kutokana na umahili na ubora wa waendesha mashtaka waliopo kwenye taasisi hiyo lakini pia kufanyika uchunguzi ulio bora.


MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم