Watu 200,000 wapatiwa Chanjo ya Uviko 19 Maswa, Elimu yaendelea kutolewa.

Fatuma Mahendeka ambaye ni Afisa Msimamizi kutoka Tanzania Development Information Organization(TADIO), akitoa somo katika kikao cha wadau wa afya wilayani Maswa.

 

Kikao cha wadau wa afya kikiendelea 

 

Kikao cha Wadau wa afya kikiendela wilayani Maswa.



Na Anita Balingilaki, Maswa

ZAIDI ya watu laki mbili wilayani Maswa mkoani Simiyu tayari wamepata chanjo ya uviko 19 huku elimu ikiendelea kutolewa kwa wananchi wengi waliobaki ili jamii nzima ipate kinga dhidi ya ugonjwa wa corona.

Hayo yamesemwa na mratibu wa huduma za chanjo wilaya ya Maswa Abel Machibya kwenye kikao kilichowahusisha maafisa afya na waandishi wa habari ambacho kimewezeshwa na internews kupitia Tanzania Development Information Organization(TADIO).

Lengo la kikao hicho ni kuboresha njia zilizokuwa zikitumika awali ili kujua sehemu gani ilikosewa,sehemu gani ilipatiwa na wapi pa kuongeza nguvu  ili kuweza  kuongeza watu ambao watakuwa tayari kupata huduma ya chanjo uviko 19.

Machibya amesema katika kufanikisha zoezi la chanjo ya uviko19  wao (wataalamu wa afya)  wamejipanga kuhakikisha wanawafikia watu wote na mpaka sasa lengo walilopewa na taifa limekamilika kwa asilimia 100 huku akiongeza kuwa asilimia walioifikia aimaanishi kuwa watu wote wamechanjwa.

“ hii tulichanja kwa lengo la taifa la kufikia asilimia 60 ya wakazi wa wilaya hii,wilaya ya maswa ina zaidi ya watu laki tano na waliochanjwa ni laki mbili na ishirini na moja, ndio wamepata chanjo, na katika kuhakikisha ambao hawajachanjwa halmashauri imejipanga kuendelea na uhamasishaji kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari,mikutano ya hadhara lengo likiwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kupata chanjo hii”amesema Machibya.

 Mbali na hayo amesema  watatumia wataalamu waliopo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pindi watu wafikapo kwenye vituo vyao kitu cha kwanza watapewa elimu ya umuhimu wa kupata chanjo ya uviko 19 na halmashauri imejipanga kuhakikisha inaendelea na uhamasishaji kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari,mikutano ya hadhara lengo likiwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kupata chanjo hiyo.

 “tutatumia njia ya kufanya mikutano kule wananchi walipo tutapeleka huduma za mikoba za chanjo kwenye mikutano ili kuwasogezea huduma karibu wakishapata elimu wanachanja hapo hapo, tutatumia watu maarufu mikakati hii tumejiwekea sisi halmashauri ili tuwafikie watu wetu wapate kinga madhubuti dhidi ya ugonjwa wa uviko 19.

Kuhusu mwitikio wa chanjo kwasasa na awali Machibya anasema baada ya ugonjwa huu kupunguza kasi  ya kuambukizana mwitiko kwa wananchi umeshuka kwani  wapo wanaoamini ugonjwa huu umeisha lakini kiuhalisia ugonjwa huo bado upo huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kujitokeze kupata chanjo ili watu wote wawe wamekamilisha chanjo kuwe na kinga ya jamii hata kama ugonjwa utakuwepo watu wasiwezi kuambukizana kwasababu kila mmoja atakuwa na kinga ya kutosha.

Changamoto walizokutana nazo wakati wa zoezi likiendelea Machibya amesema kuna baadhi ya watu wenye group O la damu kugoma kuchanjwa kwa kile wanachodai wao hawawezi kupata maambukizi kiurahisi  kutokana na aina ya damu waliyonayo huku akiongeza kuwa elimu zaidi inaendelea kutolewa ili wachache wenye mtazamo huo wapate chanjo kwani ugonjwa huo unampata mtu yeyote.

Fatuma Mahendeka ni afisa msimamizi kutoka Tanzania Development Information Organization (TADIO) amesema kupitia  internews wameweza kuwawezesha TADIO kuhakikisha uhamasishaji wa chanjo katika wilaya ya Maswa, kuboresha njia zilizokuwa zinatumika katika kuwahamashisha wananchi kwenda kupata chanj  sambamba na kuboresha taarifa zinazotoka kwa maafisa afya baada ya wananchi kupata chanjo.

“Baada ya kujua jinsi mradi ulivyofanyika kutoka kwa maafisa afya njia mbalimbali walizozitumia kwa kujua idadi (takwimu )ya watu ambao wamechanjwa na kiasi cha watu ambao bado hawajapata chanjo, tunaweza kujua ni njia zipi wanaweza kuziboresha kuweza kuwafikia watu wote” amesema Mahendeka.

 

Awali afisa ambaye pia ni Mratibu wa Usafi na Mazingira wilayani hapo Budodi Walwa amesema wamejipanga kuhakikisha ndani ya miezi michache wanaifikia idadi ya wananchi ambao hawajapata chanjo hiyo wilayani hapo na watatumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao watapita kaya hadi kaya kuhakikisha wanawaelimisha wananchi juu ya madhara ya uviko 19, waganga wa tiba asili na tiba mbadala ambao nao wana ushawishi katika jamii hivyo watatumika kuifikia jamii  huku maafisa afya wakitumia vyombo vya habari na mikutano kufikisha ujumbe ili jamii yote ipate chanjo hiyo.

 

MWISHO.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post