Ujenzi wa tenki la Maji lenye ujazo wa Lita Milioni mbili unaendelea katika
Kijiji Cha Hinduki wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu unaosimamiwa na MAUWASA.
Na Samwel Mwanga, Maswa.
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) iliyoko wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imeanza kutekeleza ahadi ya Waziri wa Maji,Jumaa Aweso ya Ujenzi wa tenki la kuhifadhi Maji lita Milioni mbili na ulazaji wa bomba katika tenki la Maji lenye ujazo wa lita Milioni moja.
Waziri Aweso alitoa ahadi hiyo hivi karibuni alipotembelea Mamlaka hiyo mara baada ya kuzindua Mradi mkubwa wa kutibu na kuchuja Maji ulioko katika Kijiji cha Zanzui wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias amesema kuwa tayari wameshapokea kiasi cha fedha zaidi ya shilingi mil. 350 Kwa ajili ya Ujenzi wa tenki hilo ambalo limeshaanza kujengwa katika Kijiji Cha Hinduki.
Mhandisi Nandi amesema pia tayari wameshanunua bomba zenye gharama ya Sh Milioni 250 na kazi ya ulazaji wa bomba katika tenki jipya lililoko kwenye kilima cha Nyalikungu mjini Maswa umeshaanza ambalo Lina uwezo wa kuhifadhi Maji lita Milioni moja.
"Mtakumbuka
kuwa Waziri Aweso alifanya ziara katika Mamlaka yetu ya Mauwasa aliweza
kuzindua ule mtambo wa kutibu na kuchuja Maji ambao ni mkubwa sana uliko katika
Kijiji Cha Zanzui" Amesema na kuongeza.
"Pia alitoa ahadi kuwa ataleta fedha kwa ajili ya Ujenzi wa tenki jingine kubwa la Maji lenye uwezo wa kuhifadhi Lita Milioni mbili tayari Ujenzi umeanza kama mlivyoona na lile tenki la mjini Maswa kwenye kilima cha Nyalikungu wenyewe ulishakamilika alihaidi kutuletea fedha kwa ajili ya ununuzi wa bomba za kuingiza na kutoa Maji tayari kazi imeanza ya kulaza bomba hizo,".
Amesema kuwa pindi miradi yote hiyo itakapokamilika itawasaidia wakazi wa mji wa Maswa na vijiji 11 wanaotumia maji kupitia chanzo Cha maji Cha bwawa la New Sola watapata maji ya uhakika kwa muda wa masaa 24 sambamba na kupunguza gharama za uendeshaji kwa mamlaka hiyo.
"Kwa Sasa Wananchi tunaowahudumia wanapata Maji kwa masaa 12 lakini baada ya Ujenzi wa tenki like tunalojenga huko Hinduki ukikamilika na hili tenki lililojengwa kwenye kilima cha Nyalikungu likaanza kazi hivyo Wananchi watapata maji Kwa masaa 24,"amesema.
Mhandisi Nandi ametumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuruhusu kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo inayosimamiwa na Mamlaka hiyo kupitia Wizara ya Maji.
MWISHO
إرسال تعليق