TARURA, TASAF wajenga daraja la Mawe kuwaokoa wananchi.

 
 
 
Daraja la mto Mwanzagamba lilioko kijiji cha Buganza, kata ya Mwanyahina wilayani Meatu ambalo linajengwa kwa Mawe kwa gharama ya shilingi mil 70 kupitia Mpango wa kunusuru Kaya Maskini na kusimamiwa na Wakala wa Barabara za Mjini na Vijiji (TARURA) wilaya ya Meatu.
 

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.

 

WAKALA wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) wilayani Meatu Mkoani Simiyu kwa kushirikiana na Mpango wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wameanza kujenga madaraja kwa kutumia Teknolojia ya Mawe ili kuongeza ufanisi, kupunguza gharama na kutunza mazingira.

 

Ujenzi wa daraja la Mawe unaendelea kwenye Mto Mwanzagamba ulioko Kata ya Mwanyahina wilayani humo uliokuwa kikwazo kwa Wanawake kwenda kupata huduma za afya ikiwemo kujifungua katika Hospitali ya wilaya.

 

Akizungumza juzi na waandishi wa habari wakati wa ukaguzi wa barabara zilizofunguliwa na Wakala huo, Msanifu Ujenzi kutoka Ofisi ya TARURA wilayani humo Maduhu Vicent amesema mradi huo wa ujenzi wa daraja uliibuliwa na wananchi kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

 

Amesema baada ya wananchi kuibua mradi huo, Ofisi ya Wakala huo ilifanya usanifu kulingana na gharama walizokuwa wamekusudia kiasi cha shilingi mil. 70 kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo na kwamba wanajenga daraja la mawe kutokana na mawe kupatikana kwa urahisi.

 

‘’Kulingana na mazingira haya, mawe yanapatikana kwa urahisi kwani tungesema tujenge daraja la zege, kiasi cha shilingi milioni 70 isingetosha kujenga daraja la mita 26…jamii itaanza kutumia daraja hili muda si mrefu’’ amesema Maduhu.

 

Wakazi wa kijiji cha Buganza wanaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza ujenzi wa daraja hilo kupitia Mpango wa kunusuru kaya maskini ambapo walengwa wa TASAF wananufaika kupitia ajira za muda.

 

Nsulwa Sucha Mwenyekiti wa kijiji hicho amesema wananchi waliomba mradi huo kutokana na kero ya barabara hasa nyakati za mvua kwani walimu walikuwa wanashindwa kuvuka mto ili wakafundishe kutokana na mto kujaa maji.

 

‘’Wanafunzi wa Meatu sekondari walikuwa wanashindwa kwenda shule, akina mama wajawazito walikuwa wanashindwa kupelekwa hospitali kutokana na mto kujaa maji na walikuwa wanajifungulia njiani…tunaishukuru serikali kwa kutupatia mradi huu’’ amesema Mwenyekiti huyo.

 

Naye Minza Maduhu Mkazi wa kijiji hicho alisema wakazi wa eneo hilo walikuwa wanapoteza maisha kutokana na mto kujaa maji, hivyo kupitia Mpango wa kunusuru Kaya maskini waliibua ujenzi wa daraja la mto Mwanzagamba.

 

Mratibu wa TASAF wilaya ya Meatu Rashid Pupwa amesema wanatekeleza miradi ya Elimu kwa kujenga maabara, madarasa na vyoo, Sekta ya Afya kwa kujenga zahanati pamoja na barabara miradi ambayo huibuliwa na wananchi ambao ni walengwa wa TASAF.

 

Amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa kupitia ajira za muda ambazo walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini hufanya kazi na kulipwa ujira ili kujiletea maendeleo katika maeneo wanayoishi.

 

‘’Wananchi wa Ng’ambo ya mto (kijiji cha Buganza) wanakabiliwa na changamoto ya mto, usafiri na usafirishaji wa mazao unakwama…jamii iliibua mradi huo ambao unatekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 70 ambapo Wakala wa Barabara ni wanatoa ufundi na fedha zinatolewa na TASAF’’ amesema Pupwa.

 

Ameongeza kuwa katika mradi huo, kijiji hicho kina jumla ya wanufaika wa TASAF 51, lakini kazi ya ujenzi inafanywa na wanufaika 46 wakati huo wengine wana umri mkubwa hivyo hawawezi kufanya shughuli za vibarua.

 

MWISHO. 



Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post