Nature Tanzania yatoa Elimu kuwalinda ndege Tumbusi.


MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Nature Tanzania John Salehe (kulia) akiwa na Mratibu wa Programu ya Kudhibiti Utowekaji wa viumbe kutoka Birdlife Africa Bi. Fadzai Matsvimbo, wakiongea na waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala (hawapo pichani) katika kijiji cha Mbushi, hivi karibuni.
 
 

Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.

 

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Nature Tanzania kwa kushirikiana na Serikali wameanza kutoa elimu kwa Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wilayani Meatu mkoani Simiyu ili kudhibiti ujangili wa ndege aina ya Tumbusi ambao wako hatarini kutoweka.

 

Imedaiwa kuwa ndege hao wamekuwa wakiuwawa na waganga wa tiba asili na tiba mbadala ili kupata viungo vitakavyotumika kwenye dawa za miti shamba ambazo husaidia kuwa na kumbukumbu, biashara na ndoto kwa wateja wao.

 

Akizungumza mara baada ya kutoa elimu kwa waganga hao, Afisa Mradi wa Uhifadhi wa ndege Tumbusi, kutoka Nature Tanzania, Alpha Mfilinge amesema wametafuta njia mbadala ya matumizi ya viungo vya Tumbusi wakishirikiana na kitengo cha Tiba asili.

 

Amesema baada ya kuwashirikisha kitengo cha Tiba Mbadala, walitajiwa kuwa wanatumia mmea mbadala aina ya Kiloto kipindi ambacho hawawapati ndege aina ya Tumbusi sababu wamekuwa adimu.

 

‘’Walikuja na hilo wazo la mmea aina ya Viloto ambao ni mbadala wa Tumbusi, tumeanza kwa hatua za mwanzo…mmea tumeupata na kuupeleka chuo kikuu cha Dar es Salaam na Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa utafiti, wamekubaliana na wako tayari kuutumia kama mbadala wa Tumbusi’’ amesema.

 

Amefafanua kuwa, waganga hao waliamini kuwa ndege huyo ana uwezo wa kuona mzoga hata ukiw mbali, ambapo walikuwa wanatumia ubongo wa ndege huyo kujua kesho ikiwemo wateja ambao ni wafanyabiashara.

 

Zemu Ngwesele, Mwenyekiti wa Waganga kijiji Cha Mbushi wilayani Meatu amesema baada ya ndege aina ya Tumbusi kuanza kutoweka walipata mbadala wa mti aina ya Kiloto ambap unapatikana mkoa wa Kigoma, Katavi na Mbeya na unafanya kazi sawa na viuongo kutoka kwa ndege Tumbusi.

 

Amewataka waganga kutoendelea kuwauwa ndege aina ya Tumbusi ili kulinda uhifadhi wa ndege hao ambao wako hatarini kupotea na badala yake watumie mti aina ya Kiloto au wandefala.

 

Jalucha Salu, mganga wa Tiba Asili amesema huko nyuma mababu zao walikuwa wanatumia ndege aina ya Tumbusi kama kiungo cha dawa zao, lakini kutokana na elimu ya uhifadhi waliyopewa na umuhimu wa ndege  huyo waganga hao hawawezi kuendelea kumuua.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Faudhia Ngatumbula amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kutoa elimu kwa wadau wote juu ya umuhimu na uhifadhi wa ndege aina ya Tumbusi katika Pori la Akiba Makao (WMA).

 

Amesema serikali wilayani humo itaendelea kutoa ushirikiano katika uhifadhi hususani kwa ndege aina ya Tumbusi (Mbesi) na pia kutoa elimu kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala juu ya umuhimu na faida za uhifadhi.

 

‘’kama tutafanikiwa kupata huo mmea tukauweka katika eneo letu la Meatu, tunaweza kuufanya uhifadhi kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu tutakomesha mauaji ya ndege huyo ambaye anatumika kwenye dawa za asili’’ amesema Ngatumbula.

 

MWISHO.


Waganga wa Tiba asili na Tiba Mbadala utoka kijiji cha Mbusi wilayani Meatu wakipewa elimu juu ya kukabiliana na ujangili wa ndege aina ya Tumbusi ambaye yuko hatarini kutoweka.



Viongozi kutoka Shirika la Nature Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja na Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala katika kijiji cha Mbushi wilayani Meatu mkoani Simiyu, mara baada ya kufanya kikao kujadili udhibiti wa ujangili wa ndege aina ya Tumbusi (Mbeshi).



 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم