MAUWASA yapokea Pampu za Maji kuongeza ufanisi.


 PAMPU ya Kusukuma Maji.



Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa,Raphael Mwita akizungumzia mapokezi ya pampu mpya tatu za kusukuma maji walizopokea kutoka Wizara ya Maji.


Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.

 

SERIKALI Kupitia Wizara ya Maji, imenunua Pampu tatu za kusukma maji ili kuongeza ufanisi katika Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (MAUWASA) iliyoko wilayani Maswa mkoa wa Simiyu.

 

Pampu hizo ambazo zimenunuliwa kwa kushirikiana na Mamlaka hiyo, ni sehemu ya pampu 16 ambazo zinapaswa kununulia ili kuboresha hali ya upatikanaji wa Maji katika mji wa Maswa na Vijiji vipatavyo 12.

 

Akizungumza ofisini kwake, mara baada ya kupokea pampu hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA, Raphael Mwita alisema kuwa pampu hizo ni sehemu ya uboreshaji wa huduma ya Maji inayotolewa na Mamlaka hiyo.

 

Alisema kuwa  pampu 16 zilizopo ni za muda mrefu na kwa sasa zimechakaa  na ufanisi wake wa utendaji wa kazi umeshuka hadi kufikia asilimia 40 na kwamba Pampu zilizonunuliwa zitafungwa kwenye mitambo ya kusambaza Maji iliyoko katika bwawa la New Sola (Bwawa la Zanzui) ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji cha Mamlaka hiyo.

 

"Tunazo pampu 16 katika mitambo yetu ya kusukuma maji kutoka bwawani kwenda kwa wananchi lakini pampu hizo ni za muda mrefu tangu zifungwe mwaka 1990 sasa ni  miaka  33 zimechakaa na hata utendaji kazi wake yaani ufanisi umepunguza kutoka asilimia 100 hadi asilimia 40," alisema Mwita.

 

Mwita alieleza kuwa kutokana na hali hiyo hata gharama za matengenezo zimekuwa kubwa pamoja na pampu hizo kutumia kiasi kikubwa cha umeme na kuongeza gharama za uendeshaji kuwa kubwa kwa Mamlaka hiyo sambamba na maeneo mengine kutopata huduma ya Maji.

 

"Pampu zikiwa chakavu ni tatizo zinatuingiza gharama kubwa ya matengenezo ya mara kwa mara na hata umeme unaotumika kuziendesha ni mwingi na hivyo Mamlaka kubeba mzigo mkubwa wa uendeshaji na Kuna baadhi ya maeneo Maji hayafiki kutokana na pampu kutokuwa na nguvu ya kutosha ya kusukuma maji," alisema.

 

Diwani wa Kata ya Zanzui, Jeremiah Shigalla (Makondeko) ameiomba Mauwasa kuhakikisha inazifunga pampu hizo haraka ili Wananchi wa kijiji Cha Zanzui waweze kupata huduma ya maji kwa muda wote pindi maji yanaposukumwa.

 

"Tumefurahi kwa jinsi serikali kupitia Mauwasa inavyowajali wananchi wa wilaya ya Maswa ili waweze kupata huduma ya Maji safi na salama kwa kutuletea pampu hizo mpya’’ alisema.

 

MWISHO.

 

Moja ya mota ya pampu ya kusukuma maji ikiwa ni sehemu ya pampu mpya tatu walizokabidhiwa Mauwasa.


 

 Maboksi yakiwa na pampu tatu zilizonunuliwa kwa ajili ya Mauwasa ili kuboresha huduma ya Maji mjini Maswa na Vijiji 12.

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم