Mbwa Mwitu waongezwa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

 


 Na Derick Milton, Serengeti.



Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI) limefanikisha zoezi la kuhamisha Mbwa mwitu wapatao 20 kutoka hifadhi ya taifa Nkomazi na kuwaleta Hifadhi ya Taifa Serengeti.


 

Zoezi la kuwaachia wanyama hao katika Hifadhi ya Taifa Serengeti limefanyika jana katika eneo la Makoma Serengeti, ambapo lengo la kuleta Mbwa Mwitu hao ndani ya Serengeti ni la kuendeleza mfumo ikolojia kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii.


 

Akishuhudia zoezi hilo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda Moronda alisema kuwa kuongezwa Mbwa Mwitu  hao ndani ya  Hifadhi  ya  Taifa Serengeti kuna manufaa katika uhifadhi  na watalii wataweza kufurahia na kushuhudia namna wanyamapori hawa wanavyowinda tofauti na ilivyozoeleka kuwaona Simba.


 

Kwa upande wake Dkt.Emmanuel  Masenga  ambaye ni Mtafiti  Mkuu  TAWIRI  na Mkurugenzi  wa  Kituo  cha  Utafiti  wa Wanyamapori Serengeti  amesema zoezi la kurejesha Mbwa mwitu  katika hifadhi ya Taifa Serengeti  ni endelevu  kutokana na  umuhimu  wa  wanyamapori  hao katika mfumo wa Ikolojia.


 

Dkt.Masenga  amesema    wataendelea kuwafuatilia mbwa hao  kupitia visukuma mawimbi  baada ya kuwaachia ikiwa ni kuhakisha  azma ya Serikali  ya kuwarejesha kwa wingi mbwa mwitu  ndani  ya  Hifadhi   ya Taifa Serengeti  inatimia kwa ajili ya kutunza bioanuwai hii isitoweke.


MWISHO.


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post