Na Derick Milton, Serengeti.
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI) limefanikisha zoezi la kuhamisha Mbwa mwitu wapatao 20 kutoka hifadhi ya taifa Nkomazi na kuwaleta Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Zoezi la kuwaachia wanyama hao katika Hifadhi ya Taifa Serengeti limefanyika jana katika eneo la Makoma Serengeti, ambapo lengo la kuleta Mbwa Mwitu hao ndani ya Serengeti ni la kuendeleza mfumo ikolojia kwa ustawi wa uhifadhi na kukuza utalii.
Akishuhudia zoezi hilo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Moronda Moronda alisema kuwa kuongezwa Mbwa Mwitu hao ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti kuna manufaa katika uhifadhi na watalii wataweza kufurahia na kushuhudia namna wanyamapori hawa wanavyowinda tofauti na ilivyozoeleka kuwaona Simba.
Kwa upande wake Dkt.Emmanuel Masenga ambaye ni Mtafiti Mkuu TAWIRI na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Serengeti amesema zoezi la kurejesha Mbwa mwitu katika hifadhi ya Taifa Serengeti ni endelevu kutokana na umuhimu wa wanyamapori hao katika mfumo wa Ikolojia.
Dkt.Masenga amesema wataendelea kuwafuatilia mbwa hao kupitia visukuma mawimbi baada ya kuwaachia ikiwa ni kuhakisha azma ya Serikali ya kuwarejesha kwa wingi mbwa mwitu ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti inatimia kwa ajili ya kutunza bioanuwai hii isitoweke.
MWISHO.
إرسال تعليق