Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
KAMPUNI ya Alliance Ginnery iliyoko Kasoli wilayani Bariadi Mkoani Simiyu ambayo hujishughulisha na Ununuzi wa Pamba nchini, kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali ya CQuestCapital na For Women Foundation wamejenga na kukabidhi wodi ya wakina mama yenye thamani ya shilingi milioni 79 katika kijiji cha Mwamlapa wilayani Bariadi Mkoani Simiyu.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa jengo hilo, Meneja wa Alliance Ginnery Boaz Ogolla alisema huko nyuma wananchi wa kijiji cha Mwamlapa walichangishana ili kukamilisha ujenzi huo lakini hawakuweza kufanikiwa.
Amesema, kujengwa kwa wodi hiyo ni ushindi kwa wananchi na kwamba jengo hilo limekamilika kwa asilimia 100 kutokana na ushirikiano baina ya viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wananchi.
Amesema, lengo lilikuwa ni kujenga wodi ya wakinamama kwa muda wa miezi mitatu, lakini kutokana na mchangowa nguvu kazi ya wananchi, jengo hilo limefanikiwa kukamilika ndani ya miezi miwili na limegharimu kiasi cha shilingi mil. 79.7.
‘’Ujenzi utaeleta ufanisi wa kupunguza adha ya wakinamama kukosa mahali ya kujifungulia, kuboresha huduma za afya kwa akina mama wanaokwenda kujifungua…tukilitunza vizuri tutalinda afya ya mama na mtoto na pia kuna fursa ya ajira kwa wauguzi na wahudumu wengine’’ amesema Ogolla.
Amewataka wananchi kutambua kuwa jengo hilo ni la kwao wanao wajibu wa kulitunza na kululinda ili liweze kudumu na kunufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Akizungumza kabla ya kufungua wodi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dk. Yahaya Nawanda amewataka wananchi kulitunza jengo hilo ili wodi ya akinamama iweze kukaa kwa muda mrefu na wananchi waone faida ya jengo hilo.
Amesema jengo hilo lina vitanda saba kwa ajili ya kujifungulia, huku akimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi (Khalid Mbwana) kuhakikisha anaongeza vitanza sita ili kurahisisha utoaji wa huduma.
‘’Sisi kama serikali tumepokea mradi huu na tutaendelea kuutunza, kuna vitanza 7, ili wodi ifanye kazi vinahitajika vitanda 6…Mkurugenzi hakikisha ndani ya mwezi mmoja mmeleta vitanda ili wodi hii ifanye kazi kwa asilimia 100.’’ Amesema Dk. Nawanda.
Kwa upande wao wananchi wameipongeza kampuni ya Alliance Ginnery kwa kuwajengea wodi ya akina mama jambo ambalo limewaondolea adha ya kutembea mwendo mrefu kufauata huduma ya kujifungua.
Maria John Kachwele mkazi wa Mwamlapa amesema wakati hakuna wodi hiyo, wakina mama walikuwa wanatembea kilometa 30 kwa ajili ya kupata huduma ya kujifungua, ambapo aliipongeza kampuni hiyo kwa kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu.
MWISHO.
إرسال تعليق