Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kimewataka wakulima wa Pamba kuwa wavumilivu wakati serikali ikitatua changamoto ya bei ya pamba iliyojitokeza msimu huu 2022/23 kwa kujenga kiwanda cha vifaa tiba wilayani Maswa.
Itakumbukwa kuwa bei ya pamba katika msimu wa 2021/22 ilinunuliwa kwa shilingi 2100 kwa kilo moja, lakini msimu huu wa 2022/23 imenunuliwa kwa shilingi 1060.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika wilaya za Maswa na Meatu, kwenye ziara ya Umoja wa Wanawake (UWT) Taifa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed amesema serikali ya awamu ya sita imekuja na mkakati wa kujengwa kiwanda cha vifaatiba vitokanavyo na pamba ili kutatua changamoto hiyo.
Amesema miaka miwili iliyopita kulikuwa na changamoto ya bei ya pamba, ambapo mwaka jana bei ilipanda na msimu huu bei imeshuka kwenye soko la dunia na kusababisha wakulima kuuza pamba yao kwa bei ndogo.
‘’Chama Cha Mapinduzi na serikali sikivu ya Rais Samia, tumekuja na mkakati wa kuweza kutatua bei ya pamba isishuke kwa kutegemea soko la dunia…tumemwomba Rais Samia tupate kiwanda cha vifaa tiba’’ amesema na kuongeza.
‘’wilaya ya Maswa tumepata bahati ya kiwanda, ambacho wameshapewa ekari 102 na mwekezaji ni mchina atakuja kuanza ujenzi hivi karibuni, tuiombe serikali iharakishe ujenzi huu ili mwakani wakulima wauze kwa bei nzuri’’.
Anamwomba Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa ambaye pia ni MNEC Zainab Shomari, kumfikishia Rais Samia salamu za wananchi wa Simiyu, huku akimtaka kuweka msisitizo ili ujenzi wa kiwanda hicho uanze mara moja.
Anaongeza kuwa kiwanda hicho kikijengwa, wakulima watanufaika moja kwa moja kwa kuondokana na walanguzi wa pamba (machinga) kwa sababu watakuwa wanauza kiwandani na kwamba wanateseka kwa sababu ya machinga na siyo CCM.
Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa na MNEC, Zainabu Shomari amewataka wananchi kuendelea kuimini serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayotatua changamoto zao usiku na mchana.
Amesema, serikali kwa kushirikiana na CCM wanatambua changamoto za wakulima na wananchi wote, hivyo wataendelea kuzitatua kadri ya upatikanaji wa fedha.
‘’Wananchi tuendelee kuiamini serikali ya CCM, kila leo tunatatua changamoto zenu ikiwemo suala la Pamba, Elimu, Maji, Umeme, Barabara na miundombinu mingine…tusidanganywe na wanasiasa wengine wakati chama kilichoko madarakani kinawaletea maendeleo’’ amesema.
Septemba 13, mwaka huu (2023) serikali kupitia Wizara ya Afya ilitangaza kupitia Gazeti la Mwananchi, Zabuni ya Ushirikiano wa pamoja ya ujenzi wa kiwanda cha vifaatiba katika wilaya ya Maswa kwa gharama ya shilingi Bil. 20.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment