Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Taifa (UWT) Mary Chatanda amesikitishwa na namna ya utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Veronica Vicent Sayore ambaye amekuwa akikiuka maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Chatanda ameyazungunza hayo mapema leo alipokuwa akiagana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega sambamba na watumishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega mara baada ya kukamilisha ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Amewataka watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Busega kumwelekeza Mkurugenzi huyo kufanya kazi vizuri kwa kushirikiana na watumishi wenzake na pia kufuata maelekezo yanayotolewa na viongozi wa CCM.
''Mwambie Mkurugenzi asimame vizuri, ashirikiane na Chama, hayuko vizuri...mnanielewa?, ashirikiane na wenzake ashirikiane na Chama, naelewa, Mwambieni Mkurugenzi ili sisi wenye Ilani tusimame imara kuhakikisha tunasimamia Ilani iende vizuri'' amesema na kuongeza.
"Nimesikitishwa sana na tabia ya Mkurugenzi wa hapa Busega amekuwa sio mtu wa kushirikiana na wenzake, hili suala halikubaliki kwani viongozi wa Chama ndio wenye Ilani ya CCM hivyo basi anapashwa kuwa shirikisha kwenye kila suala linalohusu maendeleo kwenye Wilaya hii"
Amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia inatafuta fedha ili kuwaletea wananchi maendeleo ambapo viongozi wanatakiwa kuzisimamia ili ziweze kuleata tija kwa wananchi.
Amewataka watendaji kuendelea kusimamia miradi ya maendeleo ili fedha hizo zisichezewe na baadhi ya watu, huku akiwataka kurekebisha baadhi ya hitilafu zilizojitokeza katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.
''Miradi inapopelekwa kwenye vijiji, ni vizuri viongozi vijiji hivyo na wa Chama wakajua kuwa kuna mradi umepelekwa hapo ili wawataarifu watu waweze kuusimamia vizuri kwa sababu ndio wenye watu'' amesema.
Mwenyekiti wa UWT Taifa amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku moja Wilayani Busega ambapo ameendelea na ziara yake katika ya Wilaya ya Bariadi kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
MWISHO.


Post a Comment