Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.
Upatikanaji wa huduma za Afya Umeendelea kuimarika katika vijiji vya Nyaluhande, Mwagindi na Mwamkala Kata ya Nyaluhande wilayani Busega, Mkoani Simiyu baada ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Nyakuhande kwa gharama ya shilingi Mil. 581.4.
Makamu Mwenyekiti wa UWT MNEC. Zainab Shomari ametembelea ujenzi wa kituo hicho wakati akikagua Utekelezaji wa Ilani na kuonyeshaa kuridhishwa na ubora wa majengo na matumizi ya fedha hizo zilizotokana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
‘’Ujenzi wa kituo hiki cha Afya ni moja ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, tuendelee kujitolea na kuunga mkono juhudi za serikali, CCM imeelekea kutoa matibabu bora kwa wananchi wake…tunamshukuru Rais Samia kutuletea kituo cha Afya hapa Nyaluhande’’ alisema na kuongeza.
‘’Niombe sana wananchi tuutunze mradi huu kwa sababu ni mali yetu, msimamie vizuri zaidi ili thamani ya fedha iendane na ujenzi…pia mpeleke watoto na wakinamama kupata chanjo na huduma za kliniki na uchunguzi zaidi wa afya zetu’’.
“Azma ya serikali yetu ni kusogeza huduma muhimu za afya,ambazo zitapunguza vifo vya wagonjwa ikiwemo watoto wachanga na mama wajawazito” amesema Makamu Zainab
Zacharia Bugalika, mkazi wa kijiji cha Nyaluhande alisema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwajengea kituo cha afya Nyaluhande na kuifanya jamii kuendelea kuwa na Imani na serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi.
‘’Kazi aliyoifanya Rais Samia ni kubwa sana, mradi huu umeleta manufaa makubwa na maendeleo katika kata yetu…tunamshukuru sana na wakinamama hawatahangaika kupata huduma, bali wataipata karibu na makazi yao’’ alisema Bugalika.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Fundi Sanifu wilaya ya Busega Annastazia Mathias amesema katika kipindi cha mwezi Aprili 2022, Kata hiyo ilipokea shilingi mil. 581.4 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kutoka Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Amesema kupitia fedha hizo, wanatekeleza ujenzi wa jengo la Wagonjwa wan je (OPD), nyumba ya mtumishi, jengo la maabara, upasuaji na wodi ya wazazi.
Amefafanua kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 96 na jumla ya shilingi mil. 566 zimetumika, wakati huo ushiriki wa asilimia 10 ya nguvu za wananchi ni shilingi mil. 46.5 ambazo wamechangia.
MWISHO.
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na MNEC Zainabu Shomari (wa tatu kulia) akiwa ameambatana na baadhi ya viongozi wa CCM mkoa wa Simiyu wakitembelea ujenzi wa kituo cha Afya Nyaluhande.




Post a Comment