Rose Mathias; Mlemavu wa Viungo anayetumia Mdomo Kuchora, Kuandika.

Rose Mathias (16), Mkazi wa kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi Mkoani Simiyu ambaye ni Mlemavu wa viungo akichora picha na kuandika kwa kutumia mdomo.


   .Anahitaji kitimwendo atimize ndoto ya Elimu.  

·Wazazi wanatumia ndoo mbadala wa kiti.

 

Na COSTANTINE MATHIAS.

 

‘’Natumia mdomo kuchora na kuandika, nafundishwa na watoto wenzangu…nimeshindwa kwenda shule kutokana na wazazi kukosa fedha za kununua baiskeli ya walemavu (kitimwendo)’’, ndivyo anavyosimulia Rose Mathias (16) mkazi wa Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi, mkoa wa Simiyu.

 

Kama haujafa, hujaumbika. Ni msemo ambao kila mmoja anaweza kuutaja na kuusema kipindi anapoitembelea familia ya akina Rose Mathias, mtoto wa nne katika familia ya watoto watano wa bi. Sabina John.

 

Familia hii inakabiliwa na ugumu wa maisha kutokana na kuishi kijijini na pia hawana kipato cha kuweza kumudu mahitaji muhimu ya kila siku ya kibinadamu ikiwemo chakula, mavazi na malazi.

 

Rose anasema anatamani kupata elimu kama watoto wengine licha ya kuwa na ulemavu wa viungo ambapo kwa sasa anakabiliwa na ukosefu wa kitimwendo pamoja na ugumu ya maisha katika familia yao.

 

Anasema anapenda sana kusoma jambo ambalo linalomlazimu kuwaomba watoto wenzake wasiokuwa na ulemavu kumfundisha kusoma na kuandika kwa kutumia mdomo.

 

Anasema anatumia mdomo kushika kalamu kwa sababu mikono yake kuwa haiwezi kushika kitu chochote kwa sababu ya ulemavu na pia hutumia muda mwingi kutazama picha na kuzochora kwa kuziiga.

 

‘’Natamani na mimi kwenda shule kama wenzangu, natamani sana lakini nimeshindwa kutokana na kukosa uwezo…naishi na mama mzazi pamoja na bibi, hawana uwezo, naomba serikali inisaidie’’ anasema Rose.

 

Anaiomba serikali pamoja na wadau wa maendeleo kumsaidia kupata kitimwendo ili aweze kutembea na kutimiza ndoto yake ya kwenda shule kupata elimu jambo ambalo anaamini kuwa elimu itakomboa maisha yake.

 

Anasema kuwa mama yake mzazi amekuwa akimbeba kila siku kumtoa nje, kumwosha, kumsafisha na kumbadilishia nguo kutokana na hali ya ulemavu alionao kwa sababu yeye hawezi kutokana na mikono kukosa nguvu.

 

Mzazi wake anena, ataja kukimbiwa na Mme.

 

Sabina John, Mzazi wa Rose Mathias, anaiomba serikali na wadau wa maendeleo kumsaidia binti yake kupata kitimwendo (baiskeli ya walemavu) ili iweze kumsaidia kutembea.

 

‘’Rose ni wa kubeba kila siku kumtoa nje na kumrudisha ndani, tunaishi maisha magumu sana, tunaomba msaada kwa wasamaria wema ili tuweze kupatia fedha za kununua baiskeli au watupatie baiskeli tu’’ anasema.

 

Anaeleza kuwa endapo atapatiwa kitimwendo kitamsaidia kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine ikiwemo kanisani na shuleni ambapo kwa sasa wanambeba.

 

Anaeleza kuwa, amekuwa akimlea Rose pamoja na watoto wengine pekee yake baada ya kukimbiwa na mme wake kutokana na ugumu wa maisha ikiwemo hali ya ulemavu wa Rose.

 

‘’Mme wangu alinikimbia tangu 2011, lakini naendelea kuwalea watoto wangu akiwemo huyu Rose ambaye ni mlemavu wa viungo…naiomba serikali chini ya Rais Samia kusikia kilio change ili waweze kunisaidia hitaji la mtoto wangu’’ anasema na kuongeza.

 

‘’Sina mawasiliano na aliyekuwa mme wangu, wala sina namba yake, japokuwa nafahamu kuwa alikwenda mwambao wa Ziwa Victoria (Ng’weli)…na tangu aondoke hatuna mawasiliano’’.

 

Anafafanua kuwa amekuwa akijishughulisha na shughuli za kilimo pamoja na vibarua ili kumwingizia kipato cha kuweza kumudu hali ya maisha huku akiiomba serikali kumwingiza katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).

 

Majirani wanena.

 

Hoja Mtogwasima, mkazi wa Kasoli ambaye ni jirani anasema wanaisaidia familia hiyo hususani Mlemavu wa viungo (Rose) kwa kumpatia chakula na pia wakati mwingine kumhamisha kutoka juani kwenda kivulini.

 

‘’akipata shida anatuita, nisaidieni hapa…akiwa nje hapa tunamtoa juani, tunampa maji, tukiivisha chakula tunamleta na tunaishi vizuri na familia hii, tunaiomba serikali iweze kuwasaidia’’ anasema.

 

Amani Yombo Luchanganya, Mkazi wa Kasoli anaiomba serikali pamoja na wadau wa maendeleo kumsaidia Rose kupatiwa kitimwendo ili aweze kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

 

Anasema kutokana na hali duni ya maisha, familia hiyo imeshindwa kumununulia baiskeli ya walemavu (kitimwendo) mtoto huyo na pia wameshindwa kumpeleka shule maalumu za walemavu kwa ajili ya kupata elimu.

 

Anasema, wao kama sehemu ya majirani wanaendelea kuisaidia familia hiyo kwa kuwapatia mahitaji muhimu pindi wanapopata fedha, lakini wanashindwa kuhimilia kutokana na hali aliyonayo Rose.

 

‘’Tunaiomba serikali, viongozi wa dini, vyama vya siasa, mashirikia binafsi na wadau wa maendeleo waitembelee familia hii ili waweze kumsaidia Rose kupata elimu, ndoto yake ni kupata elimu, ndiyo maana anajifunza kusoma, kuandika na kuchora mwenyewe’’ anasema Amani.

 

Diwani afunguka.

 

Diwani wa Kata ya Kasoli, Mayala Lucas ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi anasema wanaitambua familia hiyo na wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha wanawapatia mahitaji.

 

Anasema kata hiyo inawatambua watu wenye ulemavu kwa kuwapatia misaada mbalimbali ya kibinadamu pindi fedha zinapopatikana huku wengine wakiwa ni wanufaika wa TASAF.

 

‘’Mme wa Sabina, simjui na sijawahi kumwona…familia hii ni wahamiaji kutoka kijiji cha Salama wilaya ya Magu, walikuja wakati Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeshaanza kutekelezwa, kwa hiyo siyo wanufaika wa TASAF’’ anasema.

 

Diwani huyo anaitaka jamii kuwaibua watu wenye ulemavu ili waweze kupatiwa elimu na mahitaji mengine muhimu, kuliko kuwaficha kwa sababu wanawakosesha haki zao kama binadamu wengine.

 
MWISHO.
 
 
Sabina John, Mama Mzazi wa Rose Mathias akiwa nje ya nyumba yake.
 

ROSE Mathias (16), Mkazi wa Kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi mkoani Simiyu ambaye ni mlemavu wa viungo akiwa anakula viazi nyumbani kwao.
 
 
Sabina John (kulia) ambaye ni Mama Mzazi wa Rose Mathias (16) akimwandaa mtoto wake kwa ajili ya kumbeba kumpeleka ndani ya nyumba.
 

Sabina John (kulia) ambaye ni Mama Mzazi wa Rose Mathias (16) akimbeba mtoto wake kumpeleka ndani ya nyumba.
 
 
 
 




 
 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم