Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) na MNEC Zainabu Shomari amewataka wanafunzi hususani wasichana kusoma kwa bidii kutoka na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kuwajengea miundombinu mizuri ya elimu ikiwemo madarasa, maabara na matundu ya vyoo.
Ameyasema hayo leo mara baada ya kukagua vyumba vinne vya madarasa vilivyojengwa katika shule ya sekondari Sukuma kwa gharama ya shilingi milioni 80.
Amesema Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, hivyo wanafunzi wanao wajibu wa kusoma kwa bidii na kwamba shule za serikali zimekuwa zikifanya vizuri kuliko shule binafsi.
‘’Kuna Haki na Wajibu, serikali imetimiza wajibu wake, hivyo ni haki yenu kusoma kwa bidii na kufaulu hasa wanafunzi wa kike…wanafunzi wanaanza kidato cha kwanza au cha tano wengi lakini wanamaliza wachache, niwaombe msome kwa bidii’’ amesema.
Amesema lengo la serikali kujenga miundombinu ya elimu ni kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri ili kupata wataalamu wa baadae huku akiwataka wanafunzi hao kuwaheshimu walimu wao.
‘’Mmekuja kusoma, mengine hayawahusu…hauruhusiwi kujihusisha na mapenzi katika umri wa shule sababu utapata mimba za utotoni na kuzima ndoto za kupata elimu, mawazo na fikra yakae katika elimu’’ amesema.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohamed amesema wananchi wameona namna Rais Samia anavyopenda elimu kwa kuendelea kujenga miundombinu ya elimu.
Amesema hadi sasa kila eneo yamejengwa madarasa mazuri ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki na kuondoa hali ya kuchangishana iliyokuwepo huko nyuma.
Awali Mkuu wa Shule ya Sekondari Sukuma Lucas Mazoya amesema mradi wa vyumba vinne vya madarasa umetekelezwa na serikali kuu na umewapunguzia msongamano wanafunzi madarasani pia kuongeza hali ya ufundishaji na ujifunzaji.
Amesema mradi huo umetekelezwa kwa gharama ya shilingi mil. 80 ili kuwekeza kwenye elimu ili ifikapo mwishoni mwa mwaka 2023 wanafunzi wote wanaochaguliwa wajiunge wote kidato cha kwanza.
MWISHO.
إرسال تعليق