Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, akiongoza Misa Takatifu ya Kufungua Parokia ya Shishiyu iliyopo kijiji cha Shishiyu wilayani Maswa Mkoani Simiyu.
Na Mwandishi Wetu.
ASKOFU wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, leo Jumatano tarehe 18.10.2023, ametangaza na kufungua rasmi Parokia mpya ya Mtakatifu Yohane Paul II Shishiyu, ambayo inatokana na kumegwa kwa sehemu ya Parokia ya Malampaka iliyopo Wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Ufunguzi wa Parokia ya Shishiyu umefanyika kupitia adhimisho la Misa takatifu ambayo imehudhuriwa na Mapadre, watawa na waamini kutoka maeneo mbalimbali ya Jimbo, ambao pia wameshiriki harambee ya kuitegemeza Parokia hiyo mpya, ili kuiwezesha kukamilisha miundombinu ya Kanisa ikiwemo nyumba ya Mapadre.
Askofu Sangu amemsimika Padre Gerald Luhende kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia hiyo.
Katika mahubiri yake, Askofu Sangu amesema hatua ya kuongeza Parokia mpya imelenga kusogeza huduma za kiroho kwa watu, ili watu wafuate na kumwongokea Kristo.
Amewaomba waamini wa Jimbo la Shinyanga kuendelea kuiombea Parokia ya Shshisyu, huku akiwataka mewataka waamini wa Parokia hiyo mpya kila mmoja kuwa chachu ya ustawi na maendeleo ya Parokia yao.
Kupitia Misa ya uzinduzi wa Parokia, Askofu Sangu amewaimarisha waimarishwa 128 wa Parokia hiyo mpya.
Parokia hiyo mpya ambayo ilitangazwa na Askofu Sangu kuwa Parokia teule mwaka 2016, ina jumla ya Jumuiya ndogondogo za Kikristo 56, vigango 15 na inakadiriwa kuwa na waamini wapatao 11,356.
Parokia mpya ya Shishiyu ambayo inatokana na kugawanywa kwa Parokia ya Malampaka, inalifanya Jimbo la Shinyanga kuwa na Jumla ya Parokia 38, kutoka 37 zilizopo hivi sasa.
MWISHO.
Askofu Liberatus Sangu akimkalisha kwenye kiti ikiwa ni ishara ya kumsimika Paroko wa kwanza wa Parokia ya Mpya ya Shishiyu Padri Gerald Luhende.
Waamini wa Parokia Mpya ya Shishiyu ikiwemo waimarishwa wakisindikizwa na watawa wakimpokea Askofu Sangu baada ya kuwasili katika Parokia hiyo kabla ya kutangaza rasmi kupia hadhi ya kuwa Parokia kamili.
Mwonekano wa Kanisa la Mtakatifu Yohane Paulo II Parokia ya Mpya ya Shishiyu lililopo hatua za mwisho za ujenzi.












إرسال تعليق