Sehemu ya vidole vya Ng'wanza John Mkazi wa Kilugala kata ya Nhobora wilayani Itilima Mkoani Simiyu aliyenusurika kuuwawa na mtu asiyejulikana.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
MWANAMKE Mmoja aliyefahamika kwa jina la Ng’wanza John (50), mkazi wa kijiji cha Kilugala, kata ya Nhobora wilayani Itilima mkoani Simiyu amejeruhiwa na kunusurika kifo baada ya kukatwakatwa Mapanga Kichwani, na mikononi na mtu asiyejulikana.
Tukio hilo limetokea siku ya alhamisi (Novemba 23, 2023) majira ya saa 2 usiku, nyumbani kwa mwanamke huyo ambaye alikuwa na mtoto wake mdogo na kwamba hakuweza kumtambua mwanaume aliyetekeleza tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa amelazwa wodi ya wanawake katika Hospitali ya Mji wa Bariadi (Somanda), Ng’wanza amesema baada ya kukatwakatwa mapanga alipiga yowe huku mtoto wake akikimbia kwa jirani kutoa taarifa.
Amesema baada ya kushambulia, walinyang’anya pia simu ya mkononi na kuongeza kuwa amekatwa mapanga maeneo ya kichwani na kwenye vidole vya mikono na kusababisha vidole viwili kukatika.
"Tulikuwa ndani, nikawashiwa tochi usoni nikaanzia kupigwa mapanga, ilikuwa ni saa mbili nikapiga yowe…sasa watu wakaja nilikuwa na mtoto wangu mdogo sasa alikimbia kwenda kwa jirani kuwaambia, alikuwa analia sana na kupiga yowe majirani wakaja sasa kunisaidia" ameeleza Ng’wanza.
Ameongeza kuwa, anahisi tukio hilo linasababishwa na Imani za kishirikina ambapo kuna jirani yake (hakutaka kumtaja jina) amekuwa akimtishia maisha kuwa amekuwa anasabisha vifo kwa watoto wake.
‘’Kuna jirani yangu amekuwa akinituhumu kuroga watoto wake wakati siyo kweli, kuna siku amewahi kitamkia wazi kuwa atanimaliza, niacha kuroga wanae…nahisi yeye ndiyo amesababisha haya yote’’ amesema.
Ameongeza kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusika na tukio, licha ya kuwa yeye anauguza majeraha hospitalini, ambapo aliiomba serikali kwuasaka wote waliohusika na tukio hilo ili wachukuliwa hatua.
Nsiya John, ambaye ni dada yake na Ng’wanza anasema anashangaa kuona watu wanakata mapanga binadamu wenzao bila sababua ambapo aliitaka serikali kuchukua hatua kali ili liwe fundisho kwa wengine.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilugala wilayani Itilima, Maduhu kome anaishauri Jamii kuhakikisha inabaini na kutoa taarifa kwa viongozi juu ya mgeni yoyote anayefika kijijini hapo bila utambulisho.
"Matukio haya ni mabaya ila wananchi sasa hivi nimewaambia wananchi wakae macho na kuangalia mgeni atakayekuja atoe taarifa, pia naiomba serikali kumhamisha mama huyo kijijini hapa baada ya kuwa amepona kutoka hospitali" amesema Kome.
Diwani wa Kata ya Nhobora, Mbuke Ndaki amesema anasikitika kuona mwanamke mwenzao anafanyiwa ukatili na kijinsia wakati serikali inapambana vikali kutokomeza ukatili.
Alisema anamfahamu Ng’wanza kwamba alikwa nguvu kazi katika kijiji hicho na pia alikuwa akifanya shughuli za kilimo na kulea familia yake na kuiomba serikali kumtafutia hifadhi baada ya kuwa amepona.
"Kwa kweli yule mama kwanza makusudio ilikuwa ni kuua ila Mungu amesaidia, amepona tunakemea sana hilo tukio lililofanyika kwenye kata yangu…sijafurahishwa, mimi ni mama na aliyekatwa ni mama na yule mama ni nguvu kazi ya wanawake wenzangu, alikuwa anaisaidia familia yake alikuwa akilima analea watoto anapikia watoto anaangalia wajukuu lakini kwa hali iliyompata mama kweli inasikitisha’’ amesema na kuongeza.
‘’sisi wanawake imetusikitisha sana, niiombe tu serikali yule mama akipona umpeleke ikamhifadhi sehemu nyingine maana yake wale waliondoka na simu yake walipokuwa wakipigiwa walikuwa wanasema kwamba bado tunarudi kwenye kiporo chetu kama kuna sehemu ya kumhifadhi imsaidie yule mama ili kumsaidia’’.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Bariadi (Somanda) Dkt. Rosemary Mushi amekiri kumpokea mama huyo ambaye alikuwa na majeraha sehemu za mikono na kichwani.
"Tunakiri tulipokea majeruhi alikuwa na majeraha mbalimbali mikononi na kichwani na alipatiwa matibabu hali yake kwasasa anaendelea vizuri na yupo wodini" amesema.
MWISHO.
Ng'wanza John Mkazi wa Kijiji Cha Kuligala akiwa ameshonwa nyuzi sehemu ya kichwani baada ya kukatwakatwa mapanga na mtu asiyejulikana.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com


Post a Comment