Na Samwel Mwanga, Itilima.
VIFAA tiba vyenye thamani ya Sh Milioni 300 vimenunuliwa kwenye Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali katika wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya katika wilaya hiyo.
Hayo yameelezwa Novemba 24 mwaka huu na Mganga Mkuu wa wilaya ya Itilima, Dr Emanuel Costantine wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa ununuzi wa vifaa tiba kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM)waliofanya ziara ya kutembelea Hospitali ya wilaya hiyo iliyoko maeneo ya Nguno ili kuona sehem.u ya vifaa hivyo vilivyonunuliwa.
Amesema kuwa katika bajeti ya halmashauri ya wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika bajeti yake ilitenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa mchanganuo kuwa Zahanati Sh Milioni 50,Vituo vya afya Sh 150 na Hospitali Sh Milioni 100.
Dr. Costantine amesema kuwa kupatikana kwa vifaa hivyo kulitokana na kuidhinishwa na vikao vya Timu ya Uendeshaji huduma za Afya Wilaya (CHMT) na Timu ya Uendeshaji Shughuli za Wilaya (CMT) na Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya wilaya ya Itilima.
Akielezea mchanganuo wa vifaa tiba vilivyonunuliwa amesema kuwa Vifaa hivyo ni pamoja na Vifaa vya Meno vyenye thamani ya Milioni 49.9,Vifaa vya macho vyenye thamani ya Sh Milioni 49.9 na Kituo cha afya Ikindilo Sh Milioni 14.
Vifaa tiba vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na kwenye Kituo cha afya Nkoma vyenye thamani ya Sh Milioni 36.8,Kituo cha afya Mwanhunda Sh Milioni 69.2, Zahanati ya Senani Sh Milioni 19.9 na Zahanati ya Tembo Longalombogo Sh Milioni 29.7 na vifaa tiba vyote vimekwisha pokelewa .
“Kwa sasa katika hospitali yetu ya wilaya ya Itilima tumeanza kutoa huduma ya kinywa na meno pamoja na huduma ya macho baada ya kupata vifaa hivi ambavyo tumevinunua baada ya kupata fedha kutoka serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu,”
“Tunahaidi kuendelea kuvitunza vifaa hivyo ili huduma iendelee kutolewa hapa wilayani kwetu na kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma za afya katika wilaya jirani.”amesema.
Amesema kuwa kiasi cha fedha sh Milioni 2.7 zilizobaki wakati wa ununuzi wa vifaa hivyo zitatumika katika mwaka wa fedha 2023/2023 na tayari kwa sasa wamepokea kiasi cha fedha Sh Milioni 400 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.
Aidha hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutokuwa na uzio,kutokuwa na barabara za kuhamisha wagonjwa (walk way)kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kutokuwa na nyumba za watumishi kwani kuna nyumba moja tu.
Mbunge wa jimbo la Itilima,Njalu Silanga amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kujali afya za wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwapatia fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.
Amesema kuwa ni vizuri kwa watumishi wa hospitali hiyo kuvitumia vifaa hivyo hasa vya macho pamoja na meno kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuweza kuboresha afya za wananchi wa wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa ikitumia fedha nyingi katika sekta ya afya kwa lengo kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Amesema licha ya hospitali hiyo kuwa na idadi ndogo ya watumishi katika kada mbalimbali hivyo amewaomba kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa wanapofika katika hospitali hiyo kupata huduma huku akimuagiza Mkuu wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha hospitali hiyo inapata watumishi wa kutosha.
“Tunajua mko wachache watumishi katika hospitali hii kwa kada tofauti tofauti hivyo niwaombe pamoja na hali hiyo fanyeni kazi zenu vizuri pia tumieni lugha nzuri za upendo kwa wagonjwa wenu,”amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda amemuomba Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa kusaidiana naye suala la kupata watumishi wa Afya katika Hospitali zote za Wilaya za mkoa huo kwani bado zina upungufu kwa kada mbalimbali.
Pia amehaidi kusimamia matumizi sahihi ya vifaa hivyo pamoja na kutatua changamoto zilizopo kwenye Hospitali huku akihaidi kusimamia kutolewa kwa huduma bora katika hospitali hiyo.
“Nikuombe mheshimiwa Mwenyekiti si orodha ya Itilima tu bali ya kimkoa nawe uweze kusukuma kwa njia zako unazojua maana kuna mahali wengine sisi hatufiki ila wewe unafika ili suala la walk way mimi pamoja na Mkuu wa wilaya ya Itilima na Mkurugenzi wa halmashauri hii tutaliweka kwenye mipango yetu na bahati nzuri na mbunge yuko hapa “
“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi nikuombe nikushukuru tena,Mheshimiwa Rais ametuletea hizo Sh Milioni 300 tumenunua vifaa tiba, mimi naomba nikuhakikishie tutatoa huduma nzuri kwa wananchi lakini watumishi ambao walioko chini yangu lugha yetu itaendelea kuwa nzuri sana na kwa sababu kutibu pia ni lugha mgonjwa ukimpa lugha nzuri kama ulivyotuasa basi sisi tutaendeleza mazuri yote na mimi nitatekeleza maagizo yako,”amesema.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsha Mohamed amemkabidhi Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt Yahaya Nawanda gari la wagonjwa lililotolewa na Serikali ambalo litatumika katika kituo cha Afya Mwanunda kilichoko katika wilaya ya Itilima.
Hafla fupi ya makabidhiano hayo yamefanyika katika kituo hicho cha afya na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) wa mkoa wa Simiyu na wilaya ya Itilima pamoja na wananchi.
MWISHO
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed akijaribu kuendesha gari la kituo cha Afya Mwanhunda wilaya ya Itilima lilitolewa na serikali.
Mbunge wa Jimbo la Itilima Njalu Silanga akipiga makofi mara baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Shemsa Mohammed kukabidhi gari la Wagonjwa jituo cha Afya Mwanhunda wilaya ya Itilima, kushoto ni Mganga Mkuu wa wilaya hiyo Dk. Emmanuel Costantine.
Gari la Wagonjwa la kituo cha Afya Mwanhunda wilaya ya Itilima.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق