Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.
ASKARI wa Hifadhi ya Wanyamapori kutoka Hifadhi ya Jamii MWA-Makao, wilayani Meatu Mkoani Simiyu, wamefanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa na nyara za serikali huku wakiwa wameingia ndani ya Pori la Akiba Maswa kinyume cha sheria kwa kutumia usafiri wa pikipiki bila kibali.
Akizungumza na waandishi wa Habari, kiongozi wa Operesheni hiyo Joel Philipo amesema walipata taarifa kutoka kwa raia wema na kuingia hifadhini kwa ajili ya kudhibiti ujangili unaofanyika mara kwa mara katika hifadhi ya Jamii- Makao.
Amesema baada ya kupata taarifa, walifuatilia na kubaini kuwa watu hao wameingia, wameua na wamehifadhi nyama za wanyamapori baada ya kufanya ujangili kwa ajili ya kuzisafirisha.
‘’Tulifika porini usiku na kufanya msako, tuligawanyika ambapo saa 5:30 asubuhi tuligundua walipohifadhi mzigo…tulifanikiwa kukamata majangili wawili na pikipiki tatu, wakiwa wamewinda pundamilia wawili, digidigi tisa na impala mmoja’’ amesema.
Ameeleza kuwa hawakufanikiwa kukamata watuhumiwa wengine baada ya kukimbia na kwamba watuhumiwa waliokamatwa, wamefikisha jeshi la polisi na watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi.
Meneja wa Jumuiya ya Makao-WMA, wilayani Meatu Mkoani Simiyu, Jeremiah Lishon amesema wamekuwa wakipata taarifa za majangili kuingia hifadhini kutoka kwa raia wema na kwamba ufuatiliaji wao umekuwa na vikwazo kutokana na kuwa na mtandao mkubwa.
Amefafanua kuwa watuhumiwa hao wanafanya uhabifu mkubwa kwa kuuwa wanyama zaidi ya kumi kwa tukio moja, na wanafanya matukio kila mara lakini wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria wanaachiwa kwa dhamana na kulisababishia taifa hasara kubwa.
‘’Tunaomba serikali ilitazame hili kwa sababu tunaumia wanyama wakitoweka kwa ujangili, wadau na asasi zingine watusadie rasilimali watu na fedha ili tuweze kukabiliana na ujangili na kuhifadhi wanyama kwa ajili ya faida ya jamii ya taifa kwa ujumla’’ amesema Lishon.
Akitoa tarifa ya tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Maulid Shaba amewataja waliokamatwa kuwa ni Samwel Dotto (28), msukuma, mkazi wa Mining’una, Mkoa wa Singida na Elikana Raphael (30), mnyisanzi, mkazi wa Mwangeza, Singida.
Anaongeza kuwa pamoja na kukamatwa na nyara za serikali, watuhumiwa hao walikutwa na panga moja, kisu kimoja, tochi mbili, honi za pikipiki na betri za sola na pikipiki tatu.
Anasema watuhumiwa hao walikuwa na pikiki aina ya kinglion yenye usajili wa MC 736, rangi nyekundu na zingine mbili aina ya Haojue zenye usajili MC 976 BZS na MC 620 zikiwa na rangi nyeusi.
MWISHO.
Meneja wa Jumuiya ya Makao-WMA, wilayani Meatu
Mkoani Simiyu, Jeremiah Lishon, akizungumzia namna walivyokamata majangili ndani ya hifadhi.
Kiongozi wa Operesheni
hiyo Joel Philipo akizungumza na waandishi wa Habari (hawapo pichani) namna walivyopambana kuwakamata majangili ndani ya hifadhi.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

Post a Comment