TAARIFA KWA UMMA
UKAMATAJI WA KILOGRAMU 3,182 ZA DAWA ZA KULEVYA
Dar es Salaam, - 27 Disemba, 2023
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata jumla ya kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine katika operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam na Iringa kati ya tarehe 5 hadi 23 mwezi Disemba, 2023. Watu saba wamekamatwa kuhusika na dawa hizo ambapo wawili kati yao wana asili ya Asia.
Kiasi hiki cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine na kilogramu 1001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya. Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani.
Aidha, dawa hizi zilizozikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai. Mbinu hii inatumika kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.
Ukiacha dawa ya heroin inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye mimea ya afyuni (opium popy) inayolimwa katika nchi za Asia na baadhi ya kutoka Amerika, dawa aina ya methamphetamine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine. Dawa hii huwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbalimbali ambayo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbalimbali za kemikali bashirifu.
Dawa hii ni hatari kwa afya ya mtumiaji, madhara yake ni makubwa na hayatibiti kirahisi kwani mtumiaji hupata madhara ya kudumu kwenye ubongo na hivyo hupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusababisha uraibu na kuathiri mfumo mzima wa fahamu.
Kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingeweza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku. Hivyo, ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa a Kulevya, inatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Mamlaka kwani mafanikio haya yametokana na ushirikiano unaotokana na wananchi wanaotoa taarifa juu ya watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo mkubwa wa maafisa wa Mamlaka katika udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya.
Pia, Mamlaka inatoa onyo kwa wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali kwani Mamlaka imejizatiti kukomesha biashara ya dawa za kulevya kwa kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Mamlaka inaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha katika kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa.
Tukishirikiana, kwa umoja wetu tutaweza kuokoa vizazi vyetu na taifa letu dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.
Imetolewa na,
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
MAMLAKA YA KUDHIBITI NA KUPAMBANA
NA DAWA ZA KULEVYA.
إرسال تعليق