Na Samwel Mwanga, Busega.
SERIKALI kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu itatumia Sh 767.5 kutekeleza mradi wa maji kata ya Kabita ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wilayani humo.
Hayo yalielezwa jana na Meneja wa RUWASA wilayani humo, Mhandisi Daniel Gagala wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa maji kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu iliyotembelea mradi huo kukagua utekelezaji wa Ilani.
Alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Ruwasa wilayani humo ilipangiwa kiasi hicho cha fedha kupitia Mfuko wa Maji (NWF) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya kwanza.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa mkataba mradi huo, Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi M/S MHAPA BUILDERSA & ROAD WORKS LTD na umeanza kutekelezwa tangu Disemba 12, 2022 na ulipaswa kukamilika Novemba 30 mwaka huu lakini upatikanaji wa fedha umekuwa changamoto iliyosababisha mkandarasi huyo kuongezewa muda wa miezi miwili hadi Januari 30, 2024.
Mhandisi Gagala alisema kuwa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 80 ya utekelezaji na Mkandarasi tayari amelipwa kiasi cha Shilingi Mil. 430.6 na endapo utakamilika utaweza kuwahudumia watu 33,389 waishiyo katika Kata hiyo yenye vijiji vya Nyakaboja, Kabita, Nyamikoma A, Nyamikoma B na Shimanilwe.
“Mradi huu utakapokamilika utawahudumia wakazi 33,389 wa Kata ya Kabita katika vijiji vyotevya Kata hiyo ambavyo ni Nyakaboja,Kabita,Nyamikoma A,Nyamikoma B na Shimanilwe ambao watapata maji safi na salama ya bomba,” alisema.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo, utaongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 7.94 na kufanya jumla ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini katika wilaya hiyo kufikia asilimia 76.96 kutoka asilimia 69.02 ya hivi sasa.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsha Mohammed aliwataka RUWASA kuhakikisha mradi huo unakamilika kulingana na muda ambao wamemuongezea mkandarasi ili wananchi wa maeneo hayo aweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Alisema kuwa ni vizuri mkandarasi akaongeza kasi ili ifikapo Januari 30, 2024 mradi huo uwe umekamilika na dhamira ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anamtua ndoo mama kichwani na ndiyo maana amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya sekta ya maji.
Alisema kuwa katika ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 imeeleza kuwa ifikapo mwaka 2025 kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inapatikana maeneo ya vijijini kwa asilimia 85 na maeneo ya mijini asilimia 95.
“Nitumie fursa hii kumpongeza Rais Dkt Samia Sulluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha nyingi za maendeleo hususan katika sekta ya maji na ninyi ni mashahidi mmeona katika mradi huu wa maji wa Kabita ametoa kiasi cha fedha zaidi ya shilingi Mil. 700 hii inadhihirisha kabisa lengo lake la kumtua mama ndoo kichwani ifikapo mwaka 2025 linatimia,”alisema.
Naye Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda alisema kuwa atahakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora unaotakiwa ili uweze kuwahudumia wananchi sambamba na kuwaomba wananchi kutunza na kuilinda miundo mbinu ya maji itakayojengwa kwenye mradi huo ili iweze kutumika na kwa vizazi vijavyo.
MWISHO.
إرسال تعليق