Washiriki wa mkutano wa kitaifa wa wadau watekelezaji wa Programu Jumuishi ya kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM) leo jijini Dodoma. |
Na Anita Balingilaki,Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee wanawake na makundi
maalum Dkt Dorothy Gwajima amewataka wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote
nchini kuhakikisha wanaweka bajeti ya utekelezaji wa programu jumuishi ya
kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM) ambayo
inatekelezwa kwenye mikoa yote ya Tanzania bara.
Maagizo hayo ameyatoa wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa wadau watekelezaji wa Programu Jumuishi ya kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT MMMAM) leo jijini Dodoma.
"Programu hii ni muhimu sana kwa ukuaji timilifu wa
mtoto na mkurugenzi atakayeshindwa kupata bajeti hiyo atakuwa anachangia sababu
zinazoweza kusababisha mtoto asiweze kukua katika utimilifu wake, dugu zangu
nimejaribu kujizungusha zungushaaaa, lakini nimeshindwa naomba niagize tu moja
kwa moja kwamba kila halmashauri ihakikishe inapata bajeti ya kutekeleza
programu hii ili ni agizo, bahati nzuri TAMISEMI wapo hapa pia wamesikia"
Dkt Gwajima
Akimkaribisha mgeni rasmi mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya
Watoto kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee, Wanawake na
Makundi Maalumu Sebastian Kitiku amesema ili kuhakikisha maeneo matano ya
ECD ambayo ni lishe, afya bora, malezi yenye mwitikio, elimu, ulinzi na usalama
wa mtoto yanafanyiwa kazi kwa uwiano huku akiongeza kuwa wizara ina
mpango wa kuanza kupima maeneo hayo kwa score card.
Awali mkurugenzi mkazi kutoka shirika la Childrens in Crossfire
Craig Ferla amesema mpaka sasa jumla ya halmashauri 70 kati ya 114
tayari zimezindua programu hiyo huku matarajio yakiwa hadi kufikia
mwezi Marchi mwakani zote zitakuwa zimefikiwa huku akiiomba serikali
kuangalia namna ya kupata bajeti itakayosaidia utekelezaji wa programu hii kwa
kasi zaidi.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa klabu za waandishi wa
habari Tanzani (UTPC) Kenneth Simbaya amewataka wadau wa watoto kwa umoja wao
kuona umuhimu wa kuwatumia waandishi wa habari katika shughuli zao ili
kuipa jamii haki ya kupata habari/taarifa na kwa kufanya hivyo kutachochea
uwajibikaji kwani waandishi ndio daraja la kuripoti ukweli na pale wanapowasema
vibaya wasichukie bali wayafanyie kazi kwa kile kilichoonekana hakijakaa
vizuri kirekebishwe kwa maslahi mapana ya taifa.
Naye mmoja wa washiriki wa mkutano huo Janeth Ringo ambaye
ni afisa mradi wa mtoto kwanza kutoka mkoa wa Simiyu unaotekelezwa
kupitia programu ya PJT MMMAM amesema kupitia mkutano huo
umewezesha kuongeza mbinu na namna bora ya ya utekelezaji wa programu hiyo.
Mkutano huo unawahusisha maafisa ustawi wa jamii, maafisa
maendeleo ya jamii, viongozi wa CSOs na waandishi vinara wa habari za watoto
kutoka mikoa yote ya Tanzania bara.
Mkutano huo umeanza Disemba 11,2023 na utamalizika
Disemba 14, 2023 jijini Dodoma ukiwa na lengo la kufanya tathimini ya
Programu hiyo ukienda sambamba na uzinduzi wa mpango maalumu wa
utekelezaji wa programu hiyo.
MWISHO.
Post a Comment