Na COSTANTINE S. KAPAGALA, Bariadi.
WANANCHI wa Kijiji cha Nyanguge, Kata ya Ngulyati wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu wamechanga kiasi cha shilingi Mil. 22 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho ili kusogeza huduma za matibabu.
Kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 4000, hutegemea kituo cha Afya Ngulyati kilichoko Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambapo wananchi hutembea umbali wa kilometa 20 kwenda na kurudi kufuata huduma ya matibabu.
Akizungumza kwenye sherehe za kukaribisha mwaka mpya (2024) na kuaga mwaka 2023, Mwenyekiti wa kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao, Mlanda Shigukulu alisema walilazimika kuchangishana fedha ili kujenga zahanati na kuwaondolea wakinamama na watoto adha ya kutembea umbali mrefu kupata matibabu.
Alisema ujenzi huo ulianza mwaka 2016 chini ya usimamizi wa uongozi wa kijiji kwa kutumia michango ya wananchi hadi kufikia hatua ya upauaji ambapo uligharimu shilingi Mli. 31.6 baada ya Mbunge wa jimbo la Bariadi Mhandisi Kundo Mathew kuchangia mabati yenye thamani ya shilingi mil. 8.
‘’Tunaishukuru serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutuunga mkono, mwaka wa fedha 2022/2023 wametupatia shilingi mil. 50 kwa ajili ya ukamilishaji…tumesimamia vema na ujenzi umekamilika kwa asilimia 95, kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa vyoo ili wananchi waanze kupata huduma’’ alisema Mlanda.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza vifo vya akinamama wajazito na watoto wachanga pia watasogezewa huduma za matibabu ambapo aliwataka wananchi hasa kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao kuendelea kushikamana kukamilisha zahanati hiyo ili wazazi na jamii yao ipate huduma kwa ukaribu.
Awali Mwenyekiti wa kijiji cha Nyanguge, Msafiri Christian aliwapongeza kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao ambao hukutana kila tarehe 1, Januari kwa ajili ya kushiriki chakula na wazazi wao wakati huo wakijadili maendeleo ya kijiji chao ikiwemo ujenzi wa zahanati.
‘’Nawapongeza sana wana kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao kwa kuunga mkono jitihada za Dk. Samia Suluhu Hassan za kuwaletea wananchi maendeleo, bila nyinyi hii zahanati isingekuwa imekamilika, kwa niaba ya kijiji nawapongeza sana…endeleeni na moyo wakujitoa ili kuleta maendeleo ya kijiji chetu, naamini siku moja mtarudi kuishi humu’’ alisema.
Nao baadhi ya wananchi walikipongeza kikundi hicho cha Wafanyabishara, Wajasiriamali, Watumishi na Wasomi wanaoishi nje ya kijiji chao kwa kurudisha fadhila kwa wazazi na wananchi kwa ujumla.
Hollo Nyanda, mkazi wa Nyanguge aliwaomba pia kusaidia vijana na wanafunzi wenye ndoto za kupata elimu na mafanikio ambao wanakosa fursa na masomo kutokana na changamoto za kifamilia ikiwemo umasikin na maisha duni.
Diwani wa kata ya Ngulyati, Mganga Ndamo aliwapongeza kwa ujenzi wa zahanati huku akimwomba Mwenyekiti wa Halmashauri (Mayala Lucas) kuweka mipango ya kujenga kituo cha Afya eneo la Nyangunge ili kuunga mkono majitoleo ya wananchi ikizangatiwa kuwa kata hiyo haina zahanati wala kituo cha Afya.
Alifafanua kuwa kata hiyo haina Kituo cha Afya kutokana na kituo kilichokuwepo awali kumegwa na kuwa kwenye eneo la Halmashauri ya Mji wa Bariadi licha ya kuhudumia wananchi wengi kutokna Halmashauri ya wilaya ya Bariadi.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Mayala Lucas aliwapongeza kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao ambao wamekuwa sehemu ya kuigwa ndani ya Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani.
Alisema tangu ashike nafasi ya uongozi, hajawahi kuona kijiji chenye ushirikiano kama Nyanguge kupitia vijana wao ambao hukutana kila mwaka kwa ajili ya kusherehekea mwaka mpya pia kujadili masuala ya maendeleo.
‘’Nawapongeza sana wana Nyanguge Mtandao, sijawahi kuona ndani ya Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani kwamba kijiji kizima kinakutana sehemu moja kula, kunywa na baadae kujadili changamoto na maendeleo ya kijiji, hongereni sana…sisi kama viongozi tunaunga mkono jitihada zenu’’ alisema na kuongeza.
‘’Tumetembelea jengo la zahanati ambalo limekamilika, mmechangia Mil. 22, Mbunge (Kundo) Mil. 8 na serikali imewaongezea Mil. 50, hongereni sana, nasi kwenye Halmashautri tumewapangia Mganga na tumetenga Mil. 22 kwa jili ya vifaa tiba kwenye zahanati zetu, lazima Nyanguge tuwazingatie ili huduma ianze mra moja’’
MWISHO.
Jengo la zahanati ya kijiji cha Nyanguge ambalo limekamilika tayari kwa kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao Mlanda Shigukulu (katikati) akiwapongeza familia ya Mzee Matagulwa (Bahame Erasto) kwa kukubali kuandaa sherehe ya kijiji kizima cha Nyanguge nyumbani kwao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Mayala Lucas (wa tano kulia) akiwa na Diwani wa Kata ya Ngulyati Mganga Ndamo (wa sita kulia) wakiwa na viongozi wa Kikundi cha Bhana Nyanguge Mtandao, mara baada ya sherehe ya kuuaga na kuukaribisha mwaka 2024 zilizofanyika kijiji cha Nyanguge kilichokutanisha kijiji kizima kwa ajili ya kula, kunywa na kujadili shughuli za maendeleo.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق