Vyumba vya Madarasa ya shule mpya ya Sekondari Ikungu.
Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.
WAKAZI wa Kijiji cha Ikungu lyambeshi wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wameiomba serikali kuharakisha usajili wa shule mpya ya Ikungu ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali wa kilometa 15 kila siku kwenda na kurudi Kasoli Sekondari.
Shule hiyo mpya ambayo ujenzi wake umekamilika, haijasajiliwa kutokana na kukosa Maabara huku madarasa, jengo la utawala, vyoo vya walimu na wanafunzi vikiwa vimekamilika.
Wakizungumza na waandishi wa Habari, wakazi wa kijiji hicho wameiomba serikali kuharakisha mchakato wa usajili ili iweze kuhudumia wanafunzi na kuwaondolea adha ya kutembea mwendo mrefu kwenda shule na kurudi.
John Lunyilija Mkazi wa Ikungu B’’ amesema wanafunzi wa sekondari Kasoli wanashindwa kuhitimu masomo kutokana na kutembea umbali mrefu huku akiiomba serikali kufungua shule hiyo ili kuwanusuru wasichana na tatizo la mimba za utotoni.
‘’Wanafunzi wanashindwa kumaliza masomo kutokana na umbali mrefu, wengine wanapigwa mimba…tunaiomba serikali iifungue shule hii ambayo imejengwa na kampuni ya ununuzi wa pamba huku wananchi wakichangia ujenzi wa vyoo’’ amesema Lunyilija.
Naye Maguha Elikana amesema wanafunzi waishia njia kutokana na umbali mrefu huku wengine wakishindwa kumaliza masomo ambapo aliiomba serikali kufungua shule hiyo ili wanafunzi wasome karibu.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ikungulyambeshi B, Edward James ameiomba serikali kufungua shule hiyo ili kuwaondolea adha wanafunzi ya kutembea umbali mrefu ambapo wanafunzi hawahitimu kidato cha nne.
‘’Wanafunzi wa kike wanaathirika zaidi kwa kutembea umbali mrefu na kusababisha kukosa baadhi ya vipindi…wanakomea vichakani na kupata ujauzito, tunaomba shule ifunguliwa kwa sababu tumekamilisha ujenzi wa vyoo vya wanafunzi’’ alisema.
Ameongeza kuwa kupitia mikutano ya vijiji walikubaliana kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya wanafunzi matundu manane ambayo yamekamilika ili wanafunzi waweze kusoma karibu na makazi yao.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bariadi Mayala Lucas amesema miundombinu ya shule ya sekondari Ikungulyambeshi imekamilika lakini wanafunzi wanatembea umbali wa kilometa saba mpaka nane kila sila siku.
‘’Kata ya Ikungu ilikuwa na shule moja ya Kasoli, watoto wanatembea umbali mrefu lakini wananchi walianza kuchangia ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, tuliomba mdau wa maendeleo (Alliance Ginnery) atuchangie, alituchangia vyumba vinne vya madarasa, vyoo vya walimu na jengo la utawala’’ amesema.
Amefafanua kuwa hadi sasa kuna vyumba vinne vya madarasa, vyoo vya walimu,vyoo vya wanafunzi matundu nane pamoja na jengo la utawala ambapo Halmashauri hiyo imetenga Mil. 50 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Maabara.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanda cha Alliance Ginnery, Boazi Ogolla amesema wanashirikiana na jamii kufanya shughuli za maendeleo katika sketa za elimu, afya, maji na barabara.
Amesema baada ya kuona wanafunzi wanatembea mwendo mrefu na kusababisha kutofanya vizuri waliamua kuwasaidia wananchi kujenga shule ya sekondari ambapo kila mwaka walikuwa wanajenga madarasa mawili mawili, jengo la utawala, vyoo na madawati.
‘’Tumejenga shule hiyo kwa gharama ya shilingi Mil.150 ili wanafunzi ambao ni taifa la kesho waweze kupata elimu…baada ya kujenga madarasa vilikuja vikwazo vya jengo la utawala, lakini tumejenga jengo la uwatala kwa shilingi mil. 75 lakini sasa wanahitaji pia maabara’’ amesema.
MWISHO.
Jengo la vyumba viwili vya madarasa Ikungu Sekondari.
إرسال تعليق