Na Samwel Mwanga,Maswa.
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu limepitisha mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025.
Awali, Afisa Mipango na Uratibu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo,Julius John akiwasilisha mapendekezo hayo katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika Februari 24 mwaka huu amesema kuwa wanakadiria kukusanya na kutumia jumla ya Sh 52,495,521,000/- ambapo kati ya hizo Sh 14,515,182,767/- ni fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo .
Amesema kuwa bajeti hiyo imekuwa na ongezeko la Sh 6,541,526,000/- sawa na asilimia 14 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2023/2024 ya kiasi cha Sh 45,953,995,000/-.
“Ongezeko hili Mheshimiwa Mwenyekiti linatokana na kuongezeka kwa fedha za mishahara ya ajira mpya na upandishaji wa vyeo kwa watumishi 107,”amesema.
Amesema mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa mwaka 2024/2025 umezingatia Dira ya Taifa ya maendeleo (2025) Sheria ya bajeti Na.11 ya mwaka 2015,mwongozo wa uandaaji wa Mpango na bajeti wa mwaka 2024/2025 uliotolewa na wizara ya fedha na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2020/2025.
Akichangia mapendekezo hayo diwani wa Kata ya Busilili,Nangale amesema katika shule ya msingi Bushitala yenye wanafunzi zaidi ya 1000 lakini ina matundu ya choo saba tu hali ambayo ina hatarisha afya za wanafunzi hao wanapokuwepo shuleni hivyo ameomba shule hiyo iongezewe matundu ya vyoo kutoka 12 yaliyowekwa kwenye mapendekezo ya bajeti hiyo hadi matundu ya vyoo 24.
Naye diwani wa Viti Maalum,Witnes Philipo amesema kuwa ni vizuri Mamlaka ya Mji mdogo wa Maswa iwekewe bajeti ya kutosha ili iweze kufanya kazi zake na kuondoa migogoro inayojitokeza ya mara kwa mara kati ya Mamlaka na Halmashauri ya wilaya.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Paul Maige amewasisitiza madiwani kuhakikisha wanawasimamia watendaji katika kata zao juu ya ukusanyaji wa mapato na kuahidi kumpa ushirikiano wa karibu kudhibiti utoroshaji wa mapato.
“Madiwani wasimamieni hao watendaji wa kata waliopewa dhamana ya kukusanya mapato kwani tukikusanya mapato yetu kwa wingi tutafikia malengo ambayo tumejiwekea katika bajeti yetu hii hasa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi,’amesema.
Aidha amesema kuwa katika mapendekezo hayo Kamati ya Mipango na fedha ya Halmashauri ya wilaya ya Maswa ilifanya maboresho ambayo ni pamoja na kuweka msawazo wa vyoo katika shule za msingi na sekondari ambazo zina uhitaji mkubwa wa vyoo kwa wilaya hiyo na siyo matundu 35 tu kama bajeti ya awali ilivyopendekeza ambapo sasamatundu 228 ya vyoo yatajengwa katika Kata 19 ambazo zina changamoto zaidi.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق