Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wameridhia kuvunja Mamlaka ya mji mdogo wa Maswa iliyoko kwenye halmashauri hiyo baada ya kushindwa kujiendesha tangu kuanzishwa kwake Machi 26 mwaka 2010.
Aidha, Baraza hilo pia limepitisha azimio la kuanzishwa kwa halmashauri mbili katika wilaya hiyo ambazo ni Halmashauri ya Maswa Mashariki na Halmashauri ya Maswa Magharibi
Akizungumza mara baada ya kuwasilisha azimio hilo mwishoni mwa wiki jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Maisha Mtipa alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo miaka 13 iliyopita imeshindwa kufikia malengo ambayo yaliwekwa ya kufikia hadhi ya halmashauri ya Mji.
Alisema kuwa kwa Mamlaka hiyo imeshindwa kusimamia shughuli za maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii tangu ilipoanzishwa na kupewa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ambaye alikuwa na jukumu kubwa la kutekeleza mambo hayo pamoja na kusimamia vyanzo vya mapato na matokeo yake imekuwa ikiibebesha mzigo wa gharama Halmashauri ya wilaya.
“Ukusanyaji wa Mapato, Mamlaka ya mji mdogo pamoja na kupewa vyanzo vya mapato imeshindwa kusimamia vyanzo hivyo na matokeo yake imeendelea kuwa mzigo kwa halmashauri ya wilaya kwa kugharamia shughuli za Mamlaka hiyo kama vile posho za wajumbe wa Baraza la mji mdogo, alisema na kuongeza.
“Wameshindwa kusimamia usafi wa Mji tangu kuanzishwa kwake, ukiachilia mbali miji mingine midogomidogo…Mji wa Maswa wenyewe umeendelea kuwa mchafu na kusababisha mlipuko wa kipindupindu katika maeneo kadhaa, huku wakiendelea kuajiri watumishi wa muda (vibarua) ambao ni wazee sana ambao wanashindwa kumudu shughuli za usafi katika mji huo,”.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Paul Maige alisema kuwa pamoja na kuendelea kuilea Mamlaka hiyo ili ifikie malengo ambayo yalikuwa yamekusudiwa na wananchi wa wilaya hiyo kuwa na Halmashauri ya Mji lakini imeshindwa kwa kipindi cha miaka 13.
“Mamlaka ya mji mdogo ni kipindi cha mpito kuelekea hadhi ya halmashauri ya mji ambao wananchi wa wilaya ya Maswa walitamani kufikia malengo hayo lakini hawa tuliowakabidhi jukumu hilo wameshindwa ndani ya miaka 13 hivyo hatuna budi kuivunja kwa kujibu wa sheria,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya azimio hilo kupitishwa na Madiwani wote wameridhia mpango wa kuanzishwa kwa halmashauri mbili katika wilaya hiyo ili waweze kusogeza huduma kwa wananchi kwa kuzingatia ya wilaya hiyo ni kubwa ina Kata 36 na ina majimbo wawili ya Uchaguzi la Maswa Mashariki na Maswa Magharibi.
MWISHO.
إرسال تعليق