Na Samwel Mwanga,Maswa
MVUA zinazoendelea kunyesha katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu zimesababisha kuharibu miundo mbinu ya maji inayotumiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka hiyo kutopata maji.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha MAUWASA kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa bomba la kusafirisha maji lililoko kwenye ukingo wa Mto Sola mjini Maswa limekatika baada ya ukingo wa mto huo kubomoka.
“Kufuatia kukatika kwa bomba hilo kumesababisha wananchi wa maeneo ya Mwabayanda, Hinduki, Mwadila, Maswa Girls na Nyamasaka ambao wanapata maji kupitia Mauwasa wameathirika hivyo hawatapata maji hadi hapo matengenezo yatakapo fanyika” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Pia taarifa hiyo pia imeeleza kuwa bomba la kusafirisha maji lililoko kwenye eneo la Mto Miyobo katika kijiji cha Buyubi nalo limesombwa na maji ya mvua na hivyo kusababisha maeneo ya vijiji vya Dodoma, Buyubi na Ikungulyasubi kutopata huduma ya maji.
Akizungumzia hali hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA, Leonard Mnyeti amesema kuwa kutokana na kingo za mito hiyo kupanuliwa kutokana na maji ya mvua na hivyo kusabisha kumomonyoka kwa udongo ndiko kulikosababisha mabomba hayo kukatika.
“Bomba kuu la GRP 8 la kusafirisha maji katika mto Sola na lile Bomba kuu la GRP 10 katika mto Miyobo yote haya yamekatika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika wilaya yetu ya Maswa na hivyo kingo za mito hiyo kupanuka na kutusababishia wateja wetu kutopata maji”amesema.
Mnyeti ambaye ni Meneja Ufundi wa MAUWASA amesema ili kuhakikisha kwa sasa wateja wao wanapata maji wameamua kuchukua hatua za kuhakikisha miundo mbinu hiyo yaani hayo mabomba yanatengenezwa haraka kwani hilo ni jambo la dharula huku wakijipanga kutafuta fedha ili kuhakikisha wanakosha tatizo hilo la kuharibika kwa miundo mbinu hiyo.
“Kwa sasa tunachokifanya ni kuhakikisha wateja wetu waliokosa maji kutokana na miundo mbinu yetu ya maji kuharibiwa na maji ya mvua wanapata maji na hili jambo tumelifanya kwa udharula ila kwa baadaye tunataka tukomeshe kabisa tatizo hili ili lisiweze kutokea hivyo ni lazima tutenge bajeti ya fedha kwa ajili ya kazi hiyo,”amesema.
MAUWASA inahudumia wakazi wa mji wa Maswa na vijiji 12 na miji midogo ya Malampaka, Lalago na Sangamwalugesha na chanzo kikuu cha maji ni Bwawa la New Sola (Maarufu bwawa la Zanzui) lililoko katika kijiji cha Zanzui wilayani humo.
MWISHO.
إرسال تعليق