Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wanaume wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga wamenufaika na huduma ya tohara Kinga inayotolewa kwenye vituo vya afya pamoja na Kliniki Tembezi maarufu huduma mkoba za tohara kinga inayofikisha huduma kwenye maeneo ya mbali na ambayo ni magumu kufikika.
Mafanikio hayo makubwa ya Afua ya Tohara yamebainika wakati wa ziara ya Waandishi wa Habari Wilayani Kahama iliyofanyika Februari 19 -20,2024 iliyolenga kuangalia utekelezaji wa Afua ya Tohara Kinga kwa wanaume inayotokelezwa na THPS na Afya PLUS kwa kushirikiana na serikali kupitia Mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na PEPFAR kupitia CDC.
Huduma ya tohara Kinga inayotolewa kupitia Afua ya Tohara kwa wanaume inatekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kupitia mradi wa Afya Hatua kwa kushirikiana na AFYA PLUS pamoja na Serikali kupitia Mradi wa Afya Hatua unaofadhiliwa na Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI - The U.S President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Marekani (The U.S. Centers for Disease Control -CDC).
“Tohara ni bure na haiumizi, ni salama inaleta furaha na ina manufaa mazuri,inasaidia maisha yako. Ukifanyiwa tohara nguvu za kiume hazipungui . Baada ya kufanyiwa tohara mwaka 2023 hivi sasa kwanza ninaringa kwa sababu nimekuwa msafi, ninajiamini muda wote”,ameeleza Bida.
Naye Mhamasishaji wa Tohara Kinga ngazi ya Jamii, Shaban Hamimu amesema mwitikio wa wanaume kupata tohara kinga ni mkubwa kwani hivi sasa wanaume hawana uoga wala aibu ya kufanyiwa tohara kwani wametambua faida za tohara kinga.
Afisa Mradi wa Afya Hatua kutoka Shirika la AFYA PLUS Shinyanga, Joel Andwilege anasema Kliniki Tembezi ya Tohara Kinga imesaidia sana kuwafikia wanaume wenye umri mkubwa waliopo kwenye maeneo ambayo hakuna huduma za tohara ambapo kwa siku wanatoa huduma kwa wanaume 10 hadi 20 kutokana na eneo husika.
Huduma za tohara zikiendelea kutolewa ndani ya gari maalumu la Kliniki Tembezi ya Tohara kwa wanaume“Katika Kliniki tembezi ya Tohara Kinga huduma zote zinazopatikana kwenye vituo vya afya zinapatikana. Tunaenda kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya wanaume, migodini, kambi za wakulima na maeneo ya pembezoni na tunatoa huduma hadi nyakati za usiku ili kuwapa nafasi wanaume ambao hawapati muda kuja nyakati za mchana na kulinda usiri kwa wateja wetu ambao wanaona aibu, hawapendi kuonekana wamepatiwa huduma”,amesema Andwilege.
Kwa upande wake, Mtoa huduma za tohara katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama, Hadji Sued amesema vijana wenye umri kuanzia miaka 15 wamekuwa wakiletwa na wazazi wao kupata huduma za tohara kinga kutokana na hamasa kubwa zinazofanyika kwenye shule.
Meneja Mradi wa Afya Hatua wa THPS Mkoa wa Shinyanga Dkt. Amos Scott ameishukuru PEPFAR kupitia CDC na Timu ya Usimamizi wa huduma za Afya ya Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano wanaoutoa kwani tangu waanze kutekeleza mradi wa Afya Hatua mwaka 2021 kumekuwa na mafanikio makubwa ambapo uhamasishaji wa tohara kinga umekuwa mkubwa.
Ameeleza kuwa, THPS kupitia Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua imesaidia upatikanaji wa huduma za tohara kinga ya hiari kwa wanaume (VMMC) kama moja ya afua za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) katika mikoa ya Kigoma na Shinyanga tangu Oktoba 2021.
Dkt. Scott amesema THPS inashirikiana na AFYA Plus kutekeleza huduma za tohara katika Halmashauri zote sita mkoani Shinyanga, lengo likiwa ni kuongeza na kuendeleza ubora na usalama wa utoaji wa huduma za tohara kinga kwa vijana na wanaume wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ili kufikia asilimia 90% ya utoaji wa huduma hizo kwa wanaume katika Halmashauri zote zinazosaidiwa ifikapo 2026.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Kahama Dkt. Henry Sylivester amesema Afua ya Tohara Kinga kwa wanaume imekuwa na mafanikio makubwa wilayani Kahama ambapo vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kwa upande wa wanaume, wengi wamekuwa wakijitokeza zaidi kwenye huduma ya Utoaji wa huduma mkoba za tohara kinga inayoinalengazinazo lenga kufikisha huduma katika maeneo ya mbali na ambayo ni magumu kufikika.
Amesema kwa kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2023 katika Manispaa ya Kahama, wamefanikiwa kuwafikia wanaume 3962 kati ya wanaume 9186 waliolengwa kufikiwa na huduma ikiwa ni sawa na asilimia 43 ambapo ni juu ya malengo ya 25% waliyojiwekea kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024.
“Wanaume Kahama wamechangamkia huduma ya tohara Kinga. Tohara hii haina madhara ndiyo maana wengi wanajitokeza na mwitikio ni mkubwa hasa kwenye huduma Mkoba za Tohara ambako tukishirikiana na THPS na AFYA Plus tumeweka nguvu zaidi ili kuwafuata wanaume huko walipo”,ameeleza Dkt. Sylivester.
Ameeleza kuwa, hamasa ya wanaume kujitokeza kwa wingi kufanyiwa tohara inatokana na wanaume kutambua faida za tohara ikiwemo kujikinga na maambukizi ya VVU kwa 60%, kuimarisha usafi, kujikinga na magonjwa ya ngono, kukinga saratani ya uume na saratani ya mlango wa kizazi.
“Wanaume sasa wameondokana na Imani potofu kama yale madai kwamba tohara inapunguza nguvu za kiume, ngozi inayoondolewa kutumika kwa Imani za kishirikina, mtazamo kwamba baada ya kufanyiwa tohara kidonda huchukua muda mrefu kupona hivyo kuchelewa kushiriki tendo la ndoa. Kwa kweli mabadiliko ni makubwa sana kutokana na hamasa tunayoendelea kutoa”, ameongeza Dkt. Sylivester.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile Kwa kipindi cha Januari 2022 hadi Desemba 2023, afua ya tohara kwa wanaume kupitia mradi wa Afya Hatua imewafikia kwa huduma za tohara kinga jumla ya wanaume 73,927 wenye umri wa miaka 15 na zaidi kupitia kliniki za tohara 35 zinazotoa huduma za tohara na huduma mkoba zilizofanyika katika vituo 145 vya kutolea huduma za afya mkoani Shinyanga.
Amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa tatu wa mradi (2023/2024), mradi huo ulifikia jumla ya wanaume 26, 752 wenye umri wa miaka 15 na zaidi, hii ikiwa ni asilimia 29% ya lengo la mwaka huo wa fedha ambalo ni kuwafikia wanaume 91,022.
إرسال تعليق