Na COSTANTINE MATHIAS, Meatu.
JUMLA ya Maafisa Kilimo 47, kupitia Mpango wa Jenga Kesho iliyo Bora wameanza kuwafikia wakulima wa pamba ili kutoa Elimu za ugani ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea na viuatilifu kwenye vijiji vya wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari za pamba, Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wilaya hiyo Renatus Philibert alisema serikali imeendelea kutatua suala la upatikanaji wa pembejeo na mifumo ya masoko ambapo awali ukosefu wa maafisa ugani ulikuwa ukiwakwamisha wakulima kuzalisha wa pamba kwa tija.
Alisema kupitia Mpango wa BBT, serikali imeleta Maafisa Ugani 47 ambao wamesambazwa vijijini kwa ajili ya kusaidiana na Maafisa ugani wa serikali ili waweze kumwelimisha na kumfikia mkulima.
‘’Maafisa Ugani wamesambaa kwenye vijiji katika wilaya hii, wamesaidia kuhakiki mashamba na kumhudumia mkulima kulingana na mahitaji yake…wakulima wameanza kunufaika kwa kupata elimu ya vitendo moja kwa moja mashambani’’ alisema Renatus.
Aliongeza kuwa Maafisa Ugani wa BBT wamesaidia katika kuhakiki takwimu za wakulima kwani awali takwimu za uzalishaji wa pamba hazikuwa sahihi katika ugawaji wa dawa na idadi ya ekari.
Afisa Kilimo kupitia BBT, katika kijiji cha Nkoma Mainazam Kiduka alisema awali kijiji hicho kulitambuliwa kuwa na ekari 4000 za pamba ambazo siyo halisi, lakini baada ya ujio wa maafisa ugani hao wamebaini kuwa wakulima wengi walikuwa wanadanganya taarifa ili kupata pembejeo kwa wingi.
‘’Tumegundua kwamba, wakulima wengi walikuwa wanadanganya ili kupata mbegu au pembejeo, uhalisia mkulima ana ekari nne lakini anataja ekari 20 ili apate dawa nyingi…ujio wetu tumebaini hilo na sasa dawa zimeanza kuwatosha wakulima’’ alisema Mainazam.
Awali Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo wilaya ya Meatu, Thomas Shilabu alisema wilaya hiyo inatarajia kuvuna tani 42,000 katika msimu wa 2023/2024 na kwamba wameshapokea chupa (ekapaki) 555,400 na maboza (bomm spray) ili kuleta ufanisi katika kilimo cha pamba.
Alifafanua kuwa huko nyuma wakulima wengi walikuwa hawazingatii kanuni za kilimo bora cha pamba ikiwemo kuchanganya mazao, lakini kwa sasa wamepata elimu, wamepata tija na kuongeza uzalishaji.
Shilabu alimpongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza nguvu kwenye sekta ya kilimo ambapo ndani ya miaka mitatu amewapatia vyombo vya usafiri kwa ajili ya maafisa ugani ili watembelee wakulima na kuwahudumia kwa wakati.
‘’Tunashukuru Serikali ya Dkt. Samia kwa kutuwezesha bajeti ya kujenga nyumba za maafisa ugani vijijini ili waweze kuishi huko na kuhudumia wakulima, tumepata vifaa vya kupimia udongo kwenye mashamba ya wakulima ili wajue hali ya udongo wao ili kuinua kilimo na kufikia tija’’ alisema Shilabu.
Katika hatua nyingine Shilabu aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuajiri Maafisa Ugani kupita Mpango wa BBT ambao wameongeza nguvu katika utoaji wa elimu kwa wakulima wa pamba na mazao mengine.
Alieleza kuwa wataalamu hao wameshasambazwa vijijini ili kuwasaidia wakulima kulima kisasa na kuzingatia kanuni za kilimo cha pamba na kwamba serikali imeanza kupata takwimu halisi na sahihi za wakulima na mashamba yao.
MWISHO.
إرسال تعليق