Na COSTANTINE MATHIAS, Igunga.
BALOZI wa Pamba nchini Agrey Mwanri ameanza kutoa Elimu ya Upuliziaji sumu katika mashamba ya wakulima wa pamba ili kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao la pamba na kusababisha kupata mavuno kidogo.
Amewataka wakulima hao kuzingatia maelekezo ya Wataalamu wa Kilimo ikiwemo kusimamia upuliziaji wa dawa ili waweze kudhibiti wadudu wanashambulia pamba na kusababisha kupata mavuno haba.
Balozi Mwanri aliyasema hayo juzi wakati akitoa elimu juu ya matumizi sahihi ya vinyunyizi na dawa kwa wakulima wa pamba katika kijiji cha Imalanguzu kata ya Mwamakona wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
Kiongozi huyo amepiga kambi kwenye vijiji vya wilaya ya Igunga huku akitarajia kuwafikia wakulima wengine kwenye vijiji vya wilaya za Kishapu (Shinyanga), Meatu, Maswa, Bariadi na Busega (Simiyu).
Aliwataka wakulima kukagua mashamba yao mara kwa mara na kuwashirikisha maafisa kilimo ili wawaelekeze namna sahihi ya kudhibiti wadudu kama chawa jani na funza ambao wanafyonza na kuharibu vitumba.
Alisema serikali imetoa sumu za kuua wadudu wa pamba bure pamoja na vinyunyizi kwa lengo la kutumia fursa hiyo ambayo Rais Samia ametoa kipaumbele kwa wakulima ili waweze kuongeza uzalishaji na kujisimamia.
Aliongeza kuwa lengo la serikali ni kuzalisha tani Mil. Moja ifikapo 2025 ambapo Tanzania itaweza kuongeza katika uzalishaji wa pamba katika bara la Afrika na kwamba wananchi watajiinua kiuchumi.
‘’Tunapoteza pamba nyingi kwa sababu tumeshindwa kudhibiti wadudu waharibifu wa zao la pamba ikiwemo chawa jani na kidung’ata…tunatoa elimu hii kwa mkulima kutokana na kutodhibiti masalia, kanuni ya pamba inamtaka mkulima ang’oe masala yote ili kudhibiti wadudu’’ alisema Mwanri.
Mkaguzi wa Pamba kutoka wilaya ya Igunga, Venance Kankutebe alisema elimu inayotolewa na Balozi wa Pamba juu ya upuliziaji itawasaidia wakulima kuongeza tija ya uzalishaji.
Alisema tangu wameanza kampeni ya kuelimisha jamii juu ya namna bora na matumizi sahihi ya viua wadudu mavuno yameongezeka na mwitikio wa upuliziaji kwa wakulima na matumizi ya nozeli sahihi yamezingatiwa.
Nao baadhi ya wakulima wameipongeza serikali kwa kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya viuwatilifu huku wakiiomba serikali kutobadili vuiatilifu kila wakati.
Shija Homela Mkazi wa Imalanguzu aliiomba serikali kuendelea kutoa dawa mapema ili wakulima waweze kudhibiti wadudu wanaoshambulia pamba kwa wakati.
MWISHO.
BALOZI wa Pamba nchini Agrey Mwanri (katikati) akiwaonyesha Waandishi wa Habari (hawapo pichani) juu ya njia sahihi za upuliziaji wa sumu za kuuwa wadudu wanaoshambulia zao la pamba.
Balozi wa Pamba nchini Agrey Mwanri (wa pili kushoto) akimwelekeza Afisa Kilimo wa kata ya Mwamakona wilaya ya Igunga mkoani Tabora juu ya matumizi sahihi ya kinyunyuzi kinachotumia betri.
Shija Homela Mkazi wa kijiji cha Imalanguzu wilayani Igunga Mkoani Tabora (mbele) akipulizia shamba lake la Pamba huku Balozi wa Pamba Agrey Mwanri akimwelekeza namna sahihi ya upuliziaji alipokuwa anafanya majaribio pamoja na wakulima.
Shija Homela Mkazi wa kijiji cha Imalanguzu wilayani Igunga mkoani Tabora akipulizia shamba lake la Pamba.
BALOZI wa Pamba nchini Agrey Mwanri (katikati) akiwaonyesha wakulima wa kijiji cha Imalanguzu wilaya ya Igunga Mkoa wa Tabora namna bora ya kupulizia sumu za kuuwa wadudu wanaoshambulia zao la Pamba.
Balozi wa Pamba nchini Agrey Mwanri akiwaonyesha wakulima wa Pamba wa kijiji cha Imalanguzu wilaya ya Igunga juu ya matumizi sahihi ya nozeli kwenye pambu ya matabi wakati wa upuliziaji.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
Post a Comment