![]() |
| Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Pamba nchini (TCB) |
Na Derick Milton, Bariadi.
Bodi ya zao la Pamba nchini (TCB) imetolea ufafanuzi wa malalamiko ya baadhi ya wakulima wa zao hilo kutoka katika mkoa wa Simiyu, ambao walidai kuwa katika zoezi la upangaji wa bei ya zao lao wamekuwa hawashirikishwi.
Katika barua ya wazi ambayo iliandikwa na wakulima hao wakiongozwa na Gunini Masunga kutoka Wilayani Bariadi kwenda kwa Waziri wa Kilimo Hussen Bashe walilalamikia mfumo wa upangaji bei.
Katika Barua hiyo wakulima hao walisema kuwa Bodi ya pamba imekuwa ikipanga bei ya zao hilo bila ya kuwaonyesha mgawanyiko wa mambo mbalimbali hadi kufikia bei halisi ya kununulia zao hilo.
“ Mh Waziri! Kwa watumishi wa umma kuna kitu kinaitwa basic na take home kwenye mshaara wao! Basic huonesha kiasa chote Cha mshaara wao kabla ya Makato na kile kinachobaki baada ya Makato,” ilisema sehemu ya barua hiyo.
“Mh Waziri! Na sisi wakulima tunapaswa kuelewa basic yetu maana huo ndo mshaara wetu baada ya kulima, tunaomba basic yetu tuitambue na baada ya Makato ya Amcos, Simcu,VAT, Mbegu, na Viutilifu, take home yetu inabaki ngapi? Maana Mheshimiwa imekuwa kawaida wakulima kuwa tunatangaziwa tu take home badala ya basic yetu, na hii inatupa mawazo na mshtuko mkubwa kwetu wakulima.
Akijibu Malalamiko hayo Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Marco Mtunga alisema kuwa katika zoezi la upangaji wa bei makundi yote kwenye zao la pamba, serikali, wakulima, na wanunuzi ukaa kwa pamoja na kupanga bei.
Alisema kuwa kikao cha kukubaliana bei dira ya pamba kinahudhuriwa na wawakilishi wa wakulima, Wanunuzi wa pamba, Wizara ya Kilimo na Bodi ya Pamba ambapo kinapokea wasilisho kutoka kwa wakulima na baadaye wanunuzi nao uwasilisha.
“Baada ya kupokea mapendekezo ya bei kutoka pande zote mjadala huanza kwa kupitia kigezo kimoja kimoja ili kuona uhalisia wa pendekezo la kila upande. Bei dira hufikiwa baada ya kujiridhisha vigezo vyote vipo sawa” alisema Mtunga.
“ Kwa kuwa pamba inalimwa na wakulima zaidi ya 600,000 si rahisi wakulima wote wakahudhuria kikao hicho, hivyo uwakilishi hauepukiki hoja ya undani wa bei inavyopatikana inajadiliwa kwa kina katika kikao hicho na hoja zote ulizotaja zinajibiwa,” aliongeza Mtunga.
Alisema kuwa Kwa kuzingatia umuhimu wa bei katika biashara yoyote, serikali inazingatia maslahi ya wakulima,huku akiwataka wakulima kufahamu kwamba kipato cha mkulima kinajengwa na kiasi anachozalisha kwa hekari, ubora wa pamba anayozalisha na bei atakayolipwa.
MWISHO.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

Post a Comment