Jeshi la Polisi lawahakikishia Ulinzi Watoto wenye Ualbino.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Edith Swebe (kushoto) akiwa amebeba mtoto mwenye Ualbino, akizungumza na Mrakibu Msaidizi wa Polisi kikosi cha Kutuliza Ghasia Mgeni Festus alipotembelea kituo cha Kulea watoto wenye Ualbino na Ulemavu kilichopo Lamadi wilayani Busega.
 


Na COSTANTINE MATHIAS, Simiyu.

 

JESHI la Polisi Mkoani Simiyu limesema litaendelea kuimarisha Ulinzi na Usalama wa raia na Mali zao, ikiwemo kuwalinda watu wenye Ualbino kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2025.

 

Hayo yamebainishwa leo na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi Edith Swebe wakati akitoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika kituo cha Bikira Maria Msaada wa daima, kinacholea watoto wenye Ualbino pamoja na wenye ulemavu kilichopo Lamadi wilayani Busega.

 

Kamanda Swebe amesema kuwa katika mkoa huo, hakuna kesi za mauaji ya Watu wenye Ualbino zilizoripotiwa hivi karibuni na kwamba ulinzi wa mtoto ni wa kila Mtanzania mwenye akili timamu.

 

‘’Mkoa wetu ni salama, lakini pia tutaendelea kuwalinda wenye ualbino licha ya kuelekea kwenye uchaguzi…hakuna ukatili utakaoibuka kwenye mkoa wetu, pamoja na ulinzi wa Mwenyezi Mungu sisi tumejiwekea mikakati ya kuhakikisha watu wanabaki salama’’ amesema.

 

Amesema jeshi la polisi nchini limepewa jukumu la ulinzi na usalama ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama huku akiwaonya baadhi ya wananchi wasiokuwa wema kutolijaribu jeshi la polisi.

 

Ameongeza kuwa jeshi la polisi liko imara kuhakikisha linatoa ulinzi wa kituo hicho ikiwemo kutoa misaada na mahitaji ya kibandamu ili watoto hao waendelee kulelewa.

 

Awali Mratibu wa kituo hicho, Belensi China amesema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2011 kikiwa na watoto watatu, kinalea watoto wenye Ualbino na wenye ulemavu wa aina mbalimbali ambapo hadi sasa kina jumla ya watoto 80.

 

‘’kituo hiki kinalea watoto wenye ualbino, tunaletewa walitupwa, wenye ulemavu na watoto njiti…tunaishukuru serikali pamoja na jeshi la polisi kwa kuendelea kuimarisha ulinzi katika kituo hiki’’ amesema China.

 

Mkurugenzi wa Kituo cha Bikira Maria, Sista Maria Helena amesema jeshi hilo limechora maisha mapya kwa watoto hao kwani hawajawahi kutembelewa na jeshi la polisi huku akifafanua kuwa kituo hicho ni jicho la kuwasadia watoto wenye mahitaji maalumu wakiwemo wenye ualbino.

 

‘’sisi ni jicho la kusaidia watoto hawa, Simiyu hatuna doa baya…Jeshi la Polisi limejitolea kuimarisha ulinzi katika kituo chetu hapa, nawashukuru sana’’ amesema Sisita Helena.

 

Perpetua Zakayo ambaye ni mtoto mwenye Ualbino, amelishukuru jeshi la polisi kwa kuwatembelea katika kituo hicho kwani hapo awali walikuwa wamejenga hofu kuwa wanaweza kukamatwa.

 

Askari polisi Runzebe Sungwa amesema wametembelea kituo hicho ikiwa ni sehemu ya shukrani baada ya kumaliza mafunzo ya uaskari ili waweze kuwatumikia wananchi.

 

MWISHO.

 

Baadhi ya Askari Polisi wa Mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye kituo cha Bikira Maria Msaada wa Daima kinacholea watoto wenye Ualbino na walemavu wa viungo.


Baadhi ya Askari Polisi wa Mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye kituo cha Bikira Maria Msaada wa Daima kilichopo Lamadi wilayani Busega kinacholea watoto wenye Ualbino na walemavu wa viungo.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Edith Swebe (katikati) akiwa kwenye kituo cha watoto wenye Ualbino, kilichopo Lamadi, kushoto ni Mkurugenzi wa kituo hicho Sista Helena Maria, kulia ni Mrakibu Msaidizi wa Polisi kikosi cha Kutuliza Ghasia Mgeni Festus.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi wa Polisi, Edith Swebe (wa pili kulia) akikabidhi msaada kwa Mkurugenzi wa Kituo cha Bikira Maria Msaada wa Daima Sisita Helena Maria.


Askari polisi wakiwa na watoto wenye Ualbino katika kituo cha Bikira Maria Msaada wa Daima kilichopo Lamadi wilayani Busega.


Askari polisi wakiwa na watoto wenye Ualbino katika kituo cha Bikira Maria Msaada wa Daima kilichopo Lamadi wilayani Busega.

 

Askari polisi wakiwa na watoto wenye Ualbino katika kituo cha Bikira Maria Msaada wa Daima kilichopo Lamadi wilayani Busega.

 

Mkurugenzi wa kituo cha Bikira Maria Sista Helana Maria (wa kwanza kushoto) akimzungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu Kamishna Msaidizi wa Polisi Edith Swebe alipotembelea kituo hicho pamoja na baadhi ya Maafisa wa Polisi mkoa wa Simiyu.


 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post