Mashine ya kuhesabia fedha.
Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.
VYAMA vya Ushirika (Amcos), Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu vimetakiwa kununua mashine za kuhesabia fedha ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha ambapo awali walikuwa wanahesabu na kukabidhiana fedha kienyeji.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu wa wilaya hiyo Aswege Kaminyoge wakati akiongea na wadau wa pamba wakiwemo wanunuzi, viongozi wa Amcos, Mabenki pamoja na viongozi wa serikali na kusisitiza kuwa mashine hizo zitaondoa upotevu wa fedha uliokuwa unajitokeza na kusababisha migogoro na kusababisha kesi za madai.
Amesema baadhi ya makampuni ya kununua pamba yamekuwa yakifanya udanganyifu kwa kupeleka fedha pungufu hali inayosababisha hasara na kusababisha migogoro na madai baina ya vyama vya ushirika na makampuni.
‘’Ni agizo kutoka kwa Mkuu wa wilaya, ni amri, ile mashine haina gharama, inahesabu fedha, kampuni inakuletea fedha na kusaini haujui kama ziko sahihi au vinginevyo…pawepo na mikataba madhubuti na isainiwe na pande zote mbili ili watakaokiuka mikataba hiyo wafikishwe mahakamani’’ amesema Kaminyoge.
Aliwataka wanunuzi wa pamba kutoanza kununua bila mikataba baina yao na vyma vya ushirika pamoja wahasibu ili kudhibiti upotevu wa fedha ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara na kusababisha hasara huku wengine wakikimbia familia zao.
Alisema kutokana na makubaliano hayo, hatarajii kuona katika msimu huu Amcos au kampuni yoyote kudaiwa huku akiwasisitiza kuzingatia makubaliano hayo ikiwemo uhai wa mikataba kwa ajili ya ununuzi wa pamba.
Silyvester Nkuba kutoka Kampuni ya Gaki, aliwaomba viongozi wa vyama vya ushirika kuwa waaminifu kipindi cha ununuzi ili kulinda ubora wa zao hilo badala ya kuchafua pamba na kujisababishia hasara.
Awali Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Simiyu, Godfrey Mpepo aliwataka viongozi wa vyama hivyo kusimamia ubora wa pamba na uaminifu ili kutenda haki kwa wanunuzi badala ya kumaliza msimu kwa madeni.
MWISHO.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge akiongea kwenye kikao cha Wadau wa pamba, kilichofanyika kwa ajili ya kujadili mfumo wa ununuzi wa Pamba katika msimu wa 2024/25.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

إرسال تعليق