Na Samwel Mwanga,Maswa
MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (MAUWASA) iliyoko katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu imeboresha mfumo wa usambazaji maji kwa wateja na kwa sasa imeanza kutoa huduma ya maji kwa muda wa masaa 18 badala ya masaa 12 kwa siku.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha MAUWASA na kuthibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA,Mhandisi Nandi Mathias imeeleza kuwa kutokana na Mamlaka hiyo kuboresha hali ya upatikanaji wa maji kwa wateja walioko mjini Maswa sasa watapata maji kwa muda wa masaa 18 kwa siku ikilinganishwa na masaa 12 na hilo ni ongezeko la masaa 6.
“Kuanzia leo tarehe 31/05/2023 huduma ya Majisafi na Salama mjini Maswa inapatikana kwa masaa 18 kuanzia saa 10;00 alfajiri hadi saa 4;00 usiku,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
MAUWASA imeendelea na uboreshaji wa upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo yote wanayoyahudumia na miradi imekuwa ikitekelezwa ambapo tayari tenki la kuhifadhi maji Lita Milioni moja lililojengwa katika kilima cha Nyalikungu mjini Maswa limeshakamilika na kuanza kutumika na hivyo kuongeza muda wa upatikanaji wa maji wa wananchi wa mji huo ambao ni wateja wa Mamlaka hiyo.
Pia inaendelea na ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita Milioni Mbili linalojengwa katika kijiji cha Hinduki na lilikamilika MAUWASA itatoa huduma ya maji kwa wananchi wa mji wa Maswa kwa muda wa masaa 24.
Hata hivyo MAUWASA imekuwa ikitoa huduma ya Majisafi na salama kwa wananchi katika miji midogo ya Lalago,Sangamwalugesha na Malampaka na tayari kuna miradi inatekelezwa katika maeneo hayo na maeneo mengi.
Katika mji wa Malampaka kwa sasa wanaendelea kupata maji kupitia visima virefu huku utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ukiwa umeshaanza kwani tayari Mkandarasi amekwisha kuanza kazi hiyo huku mradi wa dharula wa maji ukiwa umekamilika na wanananchi wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama.
Pia MAUWASA inavihudumia vijiji vipatavyo 15 na kwa sasa kuna miradi ya Maji inayoendelea na ujenzi katika vijiji vya Mwashegeshi (Kata ya Nguliguli), Zanzui (Kata ya Zanzui) na Buyubi (Kata ya Mwamashimba)
Bwawa la New Sola (Maarufu bwawa la Zanzui) lililoko katika kijiji cha Zanzui wilaya ya Maswa ndicho chanzo kikuu cha Maji kinachotegemewa na MAUWASA na hudumia zaidi ya watu 149,000 na mifugo 400,00.
MWISHO.

Post a Comment