TCA yafafanua kilo ya Pamba kununuliwa 1,150.

Zao la Pamba (Maarufu Dhahabu nyeupe) likiwa shambani.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

BAADA ya Serikali kupitia Bodi ya Pamba kutangaza bei elekezi ya kununulia pamba katika msimu wa 2024/25 kuwa shilingi 1,150 kwa kilo moja, Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA) kimesema bei hiyo ni halali na inaweza kupanda baada ya wanunuzi kuanza kushindana ikitegemea soko la dunia na kuboreka.

 

Imeelezwa kuwa bei ya pamba katika nchi ya Tanzania na Bara la Afrika hutegemea soko la kimataifa na kwamba wanunuzi hawawezi kwenda kinyume na mwenendo wa bei ya soko la dunia.

 

Hayo yamebainishwa juzi na Katibu wa TCA, Boaz Ogolla wakati akifafanua malalamiko ya wakulima juu ya zao la pamba kuendelea kununuliwa kwa bei ndogo tofauti na gharama za uzalishaji.

 

Amesema bei ya zao la pamba nchini Tanzania ina unafuu tofauti na bei ya nchi jirani za Kenya, Uganda, Zambia Zimbambwe na Msumbuji ambao wameongeza tija tofauti na wakulima wa Tanzania ambao tija yao ni ndogo.

 

‘’Bei haiko mikononi mwetu, kinachohitajika ni kuongeza tija na kuongeza uzalishaji ili mkulima aweze kupata kilo 1000 mpaka 1200 kwa ekari moja…tulijaribu katika mashamba darasa ya Itilima, Zanzui na Mara na kupata kilo 1500, mkulima akiongeza tija atapata manufaa na kubadilisha maisha’’ amesema Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance Ginery.

 

Anawataka wadau wote wa sekta ya pamba kushirikiana katika kuongeza tija ili mkulima aweze kupata mapato mazuri huku akifafanua kuwa changamoto ya kilimo cha pamba Afrika hakijapata uzalishaji endelevu.

 

Akielezea changamoto ya uzalishaji, ametolea mfano mwaka huu, Afrika Mashariki imekumbwa na mvua nyingi na kukosa uzalishaji huku Afrika Kusini imekumbwa na ukame na uzalishaji wao kupungua kwa kukosa mvua.

 

‘’Uendelevu na uzalishaji haujaimarika, katika miaka mitatu iliyopita yaani mwaka 2023 tulikuwa na kilo miliono 283, mwaka 2022 tulikuwa na kilo milioni 172, mwaka 2021 tulikuwa na kilo milioni 145 na mwaka 2020 kilo milioni 121…na mwaka huu itakuwa imepungua kutokana na mvua nyingi’’ amesema Ogolla.

 

Katika hatua nyingine Ogolla ameipongeza serikali kwa kusimamia mfumo wa ununuzi wa pamba kupitia vyama vya ushirika (Amcos) ambao amesema utaongeza usimamizi wa ubora wa pamba na pia kupunguza upotevu wa fedha za wanunuzi wa pamba.

 

Ameeleza kuwa wakati pamba inanunuliwa kutoka kwa mawakala wa makampuni, pamba ilikuwa inachafuliwa na pia mkulima alikuwa akiibia baada ya mizani kuharibiwa.

 

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge amewataka wadau wa pamba kutoa elimu kwa wakulima kupitia mashamba darasa ili waweze kuongeza tija badala ya kulalamikia bei kuwa ndogo.

 

Gunini Masunga, mkulima wa pamba kata ya Bunamhala ameiomba serikali kupitia upya bei elekezi ya pamba ya shilingi 1,150 kwa kilo ili iweze kumnufaisha mkulima.

 

MWISHO.

 


Furushi la Pamba likiwa tayari kwa ajili ya kuuzwa.


Wakulima wakifurahia mavuno ya Pamba wakati wakipeleka pamba yao sokoni.
 
 
 
 
 

 

 

Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post