Tani 2.2 za Dawa za Kulevya Zakamatwa Dar Es Salaam na Tanga

 

Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo
Dawa za kulevya aina ya Skanka
Dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine
***
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 2,207.56 za dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya katika mikoa ya Tanga na Dar es Salaam. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Novemba 25, 2024, na Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, miongoni mwa dawa zilizokamatwa ni skanka, methamphetamine, heroin, na dawa tiba aina ya Fentanyl. 

Amesema Dawa hizo zilipatikana katika operesheni maalum zilizofanyika katika maeneo tofauti na kwamba Watuhumiwa saba wanashikiliwa kuhusiana na dawa hizo.


 Ameongeza kuwa , Kati ya dawa zilizokamatwa, skanka ni kilogramu 1,500.6, methamphetamine kilogramu 687.76, heroin kilogramu 19.20, na chupa 10 za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl. 

"Tarehe 14 Novemba, 2024, jijini Dar es Salaam, katika wilaya ya Kigamboni, mtaa wa Nyangwale, watuhumiwa Mohamed Suleiman Bakar (40) na Sullesh Said Mhailoh (36), wote wakazi wa Mabibo, Dar es Salaam, walikamatwa wakiwa na kilogramu 1,350.4 za dawa za kulevya aina ya skanka. 

Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya nyumba aliyopanga mtuhumiwa Mohamed, ambayo aliitumia kama ghala la kuhifadhi dawa hizo. Aidha, dawa nyingine zilipatikana ndani ya gari aina ya Nissan Juke yenye namba za usajili T 534 EJC, zikiwa tayari kwa kusambazwa",ameeleza.

" Tarehe hiyo hiyo, katika mtaa wa Pweza Sinza E, wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, mtuhumiwa Iddy Mohamed Iddy (46), mkazi wa Chanika Buyuni, alikamatwa akiwa na kilogramu 150.2 za skanka, zilizokuwa zimefichwa katika maboksi ya sabuni na baadhi ya dawa hizo zikiwa zimefichwa kwenye boksi lililotengenezwa kwa bati ngumu na kupachikwa kwenye chassis ya gari aina ya Scania lenye namba za usajili wa Afrika Kusini LN87XJGP, ambalo limekuwa likitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nje ya nchi",ameongeza. 

Ameeleza kuwa vilevile, tarehe 17 Novemba, 2024, katika jiji la Tanga, watuhumiwa Ally Kassim Ally (52) na Fahadi Ally Kassim (36) walikamatwa mtaa wa Mwakibila wakiwa na kilogramu 706.96 za dawa aina ya heroin na methamphetamine. 

Baadhi ya dawa hizo zilipatikana ndani ya gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 714 EGX, huku nyingine zikibainika kufichwa kwenye nyumba aliyopanga mtuhumiwa. 

  Tarehe 19 Novemba, 2024, katika mtaa wa Kipata na Nyamwezi Kariakoo jijini Dar es Salaam, watuhumiwa Michael Dona Mziwanda (28) mkazi wa Tabata Segerea, na Tumpale Benard Mwasakila (32) mkazi wa Temeke Mikoroshini, walikamatwa wakiwa na chupa kumi za dawa tiba zenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl wakiwa nazo katika duka la M-PESA. 

Aidha, katika operesheni hizi zilizofanyika, jumla ya magari matatu na boti moja vilivyohusika katika uhalifu huo vinashikiliwa.

 Dawa zilizokamatwa ni nyingi na zingeweza kuwa na madhara makubwa kwa jamii na taifa ikiwa zingeingia mitaani. 

Dawa hizi haziathiri tu wale waliokwisha anza matumizi ya dawa za kulevya, bali pia wafanyabiashara hawa hulenga watu wengine ambao hawajaanza matumizi ili kutanua masoko yao. Walengwa wapya wanaweza kuwa mtu yeyote katika jamii au familia za Kitanzania. 

Hivyo, ni dhahiri kuwa jamii nzima inakabiliwa na hatari ya dawa za kulevya. Kadhalika, Mamlaka imebaini kuwa wahusika wa biashara haramu ya dawa za kulevya hutumia mbinu ya kupanga nyumba ambazo zinageuzwa kuwa maghala ya kuhifadhi dawa za kulevya, huku wao wakiishi katika maeneo mengine. 

Mamlaka inatoa rai kwa wamiliki wa nyumba kuwa makini wanapopangisha nyumba zao, kwani nyumba inayotumika kwa shughuli za dawa za kulevya ni kinyume cha sheria na inaweza kutaifishwa.

 Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, imeweka katazo kwa mmiliki au msimamizi wa nyumba, msimamizi wa eneo au chombo cha usafirishaji kuruhusu vitumike kwa lengo la kutengeneza, kuvuta, kujidunga, kuuza au kununua dawa za kulevya. 

Aidha, mmiliki anapojua kuwa kosa linatendeka kwenye eneo lake, anajukumu la kutoa taarifa kwa Mamlaka. 

Kushindwa kufanya hivyo ni kosa la jinai, na akitiwa hatiani, adhabu yake inaweza kuwa faini kuanzia shilingi milioni tano hadi milioni hamsini, au kifungo cha miaka mitano hadi miaka thelathini jela, au vyote kwa pamoja. Mamlakaya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inatoa shukrani kwa wananchi wanaotoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na dawa za kulevya na tunawahimiza wananchi wote kuendelea kutoa taarifa pale wanapobaini matukio yanayohusiana na biashara haramu ya dawa za kulevya. 





Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 Comments

Post a Comment

Post a Comment (0)

Previous Post Next Post