Mgogoro wa shamba waikosesha familia makazi.


Ngusa Konya (mwenye shati la Bluu), mkazi wa kijiji cha Mwabadimu kata ya Nkololo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu akiwa na familia yake baada ya kuchomewa nyumba zake na wananchi kutokana na mgogoro wa shamba.

 

Na COSTANTINE MATHIAS, Bariadi.

 

MGOGORO wa shamba uliokuwa ukiendelea baina ya wananchi wawili katika Kijiji cha Mwabadimu, kata ya Nkololo wilayani Bariadi Mkoani Simiyu umeingia sura mpya baada ya wananchi wenye hasira kali kuingilia kati kwa kubomoa na kuchoma moto nyumba alizokuwa akiishi Ngusa Konya na wake zake wanne na kuachwa bila makazi.

 

Sakata hilo limeibuka kati ya Januari 19 na 20, 2025 baada ya wananchi hao kumpigia faini Konya ya shilingi 50,000/= kutokana na usumbufu pamoja na kuwashikia panga na mshale na baada ya kushindwa kulipa, waliamua kuharibu makazi yake kwa kubomoa na kuchoma moto ili ahame kijijini hapo.

                   

Akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Imeli Sayi alisema tukio hilo limesababishwa na ugomvi wa mashamba baina ya Ngusa Konya na Ngusa Mkula ambapo Ngusa Mkula alinunua mashamba hayo kutoka kwa baba yake Ngusa Konya aliyeitwa Konya Mang'ung'u wakati huo Ngusa Konya akiwa jela baada ya kumuua mama yake mzazi.

 

Alieleza katika msimu huu wa kilimo wawili hao walilima shamba kwa pamoja na mazao yalipoanza kukomaa kila mmoja alianza kuvuna, lakini Ngusa Mkula alitoa taarifa ofisi ya Kijiji na Mtendaji wa kijiji aliripoti kituo cha polisi Nkololo na alipokamatwa alikiri mashamba hayo kuuzwa na baba yake mzazi (Konya Mang'ung'u), lakini aliporejea nyumbani kwake aliendeleza mgogoro huo.

 

"Kesi hii ilifikishwa Mahakamani, Mahakama ikaamuru shauri hilo lisikilizwe na Kamati ya Migogoro ya kata ambapo Kamati iliamuru haki apewe Ngusa Mkula...tulimwelekeza kama hajaridhika akate Rufaa, lakini aliendeleza kuvamia mashamba hayo na kuvuna Mahindi na tulishindwa kuamua na kutoa taarifa kituo cha polisi" alisema Imeli.

 

Alieleza kuwa baada ya familia ya Ngusa Konya kuvamia mashamba, ilipigwa yowe (mwano)ambapo wananchi walikusanyika na kubaini Ngusa Konya alikuwa na makosa akapigwa faini ya shilingi 50,000/= na kutokana hali iliyowalazimu wananchi kuchukua maamuzi mengine.

 

Aliongeza kuwa maamuzi ya wananchi hayakuwa sahihi kutokana na hasira walizokuwa nazo baada ya kukataa kutoa faini na kuwachukulia panga na mkuki, lakini tutahakikisha wanaendelea kuwa salama wakati suala hili likitatuliwa.

 

Mangu Kitula, Mwenyekiti wa kitongoji cha Mwababili aliyechomewa nyumba ni Ngusa Konya na aliyevamiwa kwenye mashamba ni Ngusa Mkula baada ya mashamba hayo kuuzwa na Mzee Konya Mang'ung'u na kusababisha ugomvi wa mashamba.

 

Alisema hatua ya wananchi kuchoma nyumba ni baada ya Ngusa Konya kuwachukulia silaha na wakati huo alishawahi kuhukimiwa kifungo cha miaka mitano baada ya kumuua mama yake hali iliyowafanya wananchi kubomoa nyumba hizo ili ahame.

 

"Wananchi walifanya kosa kujichukulia Sheria mkononi na kitendo cha kuchoma nyumba siyo sahihi walitakiwa watoe taarifa ngazi za juu" alisema.

 

Ngusa Konya Mkazi wa Kijiji cha Mwabadimu, alisema alivamia na Kikundi cha watu wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji wakiwa na Mapanga na mikuki na kuanza kurusha mawe hali iliyotufanya kuyakimbia makazi yetu.

 

"Walichoma na kuvunja nyumba 10, kuku 30, Nguo, vyakula na magodoro yote yameungua...nina wake wanne na watoto 10, ambapo mpaka sasa hatuna mahali pa kuishi na tunalala nje sababu nyumba zote zimebomolewa, chakula tunapewa na majirani" alisema Konya.

 

Alieleza kuwa mpaka sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa licha ya kutoa taarifa kituo cha polisi na kwamba watoto wameshindwa kwenda Shule kutokana na kukosa sare baada ya kuteketezwa kwa moto.

 

"Nashindwa kuelewa, wao wanadai Kuna mgogoro wa ardhi, lakini mimi Sina mgogoro wa ardhi na mtu yeyote...hapa tulipo hatujaokoa kitu chochote na watoto wameshindwa kwenda shule sababu nguo zimechomwa moto" alisema.

 

Chalya Ngusa, mtoto wa Ngusa Konya alisema walivamia na Kikundi cha watu na kuanza kushambuliwa na kuyakimbia makazi yao na kutoa taarifa kituo cha polisi Nkololo.

 

"Walichoma nyumba, vitanda, nguo, kuku, nguruwe ...Shuleni hatuendi sababu nguo na madaftari yameungua, tunalala nje hapahapa, tunaomba sarikali  itusaidie kutuokoa na hili janga." Alisema Chalya.

 

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoani Simiyu limewakamata watu wawili ambao ni Imeli Sayi na Mangu Kitula ambao ni viongozi wa Kijiji cha Mwabadimu wakishirikiana na baadhi ya wanakijiji kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio la kuchoma moto nyumba 10, kuharibu mali na Mifugo pamoja na kuyakatakata mazao ya Ngusa Konya.

 

Imeelezwa kuwa hadi Sasa thamani halisi ya athari ya uharibifu huo bado haijapatikana na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na mara baada ya kukamilisha upelelezi watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.

 

Aidha, Jeshi hilo linaendelea kuwasaka wale wote ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika tukio hilo la kuharibu nyumba hizo na linatoa wito kwa wananchi kuacha mara moja kujichukulia Sheria mkononi.

 

Mwisho.

 

Nyumba za Ngusa Konya zilizochomwa moto na wananchi kutokana na mgogoro wa shamba.


 

Nyumba ya Ngusa Konya, mkazi wa Mwabadimu kata ya Nkololo wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ikiwa imebomolewa na kuchomwa moto kutokana na mgogoro wa shamba.


Ngusa Konya akiwa na familia yake.


Ngusa Konya akiwa na familia yake wakiota moto baada ya nyumba zao kuchomwa moto kutokana na mgogoro wa shamba.
 
 
 
 


Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com

0 تعليقات

إرسال تعليق

Post a Comment (0)

أحدث أقدم