Na Costantine Mathias, Simiyu.
MWENYEKITI wa UWT-Taifa, Mary Chatanda amefungua Mafunzo ya Uhamasishaji wa Matumizi ya Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi 2022 kwa viongozi wanawake wa Vijiji, Mitaa na Vitongozi Mkoani Simiyu huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na weledi kuwatumikia Watanzania.
Amesema kuna Umuhimu wa viongozi Wanawake kupata mafunzo ikiwa ni mwendelezo wa Umoja wa Wanawake kutoa mafunzo kwa viongozi na Watendaji ili wapata uelewa wa pamoja kwenye kutekeleza majukumu ya msingi kwa wanawake na Wananchi kwa ujumla.
Chatanda ameyasema hayo leo (Feb 19, 2025), wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea Uwezo wa kutekeleza majukumu yao, yaliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), katika ukumbi wa Makuti Longue mjini Bariadi.
Amesema lengo la mafunzo hayo kwa wanawake viongozi wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji ni kupata nyenzo muhimu kwenye kutekeleza majukumu yao na kwamba lengo la UWT ni kuhakikisha kiongozi mwanamke anatekeleza vema majukumu yake na kuwa mfano na kimbilio la Wananchi.
"Leo tutajifunza matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na makazi ya mwaka 2022 pamoja na mambo mengine muhimu...tutumie mafunzo haya kama fursa ya adhimi ya kujifunza na kutoa mchango wa mawazo yatakayoleta tija kwani majukumu yenu yatatumia sana takwimu" amesema Chatanda.
Amesema mafunzo hayo yatawasaidia Wanawake kushirikiana na Chama na Jumuiya zake kuwaletea Maendeleo na kuunga Mkono jitihada za Serikali ya Dk. Samia Suluhu Hassan.
Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohammed amesema CCM imewapa nafasi kubwa Wanawake kuwania nafasi kubwa ya Uongozi hali iliyowafanya Wanawake wengi kushinda kwenye Uchaguzi wa serikali za Mitaa, vijiji na Vitongoji.
Amesema kuwa CCM itahakikisha inafanya kazi na Wanawake viongozi pamoja na kuwajengea uwezo ili wafanye kazi kwa misingi na weledi katika kuwatumikia wananchi ambapo waliwaweka madarakani.
Mwakilishi wa Mtakimu Mkuu wa Serikali, Benedict Mgambi wanatoa mafunzo ya Uhamasishaji wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ili iwe chachu ya Maendeleo kwa viongozi hao.
"Tunatoa mafunzo haya ili yatuongezee maarifa na tuweze kufanya kazi katika Mitaa, vijiji na Vitongozi vyetu kwa kujua idadi ya watu na makazi yao" amesema Benedict.
Limi Silanga, Mwenyekiti wa mtaa wa Majahida amesema semina hiyo itasaidia viongozi wapya na wale wa zamani kujenga uelewa wa pamoja katika kuwatumikia wananchi.
Naye Veronika Masunga, Mwenyekiti mtaa wa Ilalambuli amesema semina hiyo inawafaa sababu watazijua takwimu za watu na makazi na watafanya kazi bila kuwabagua wananchi.
"Tumesisitizwa kuwa kiongozi anayekilisha wananchi hatakiwi kubagua wananchi, anatakiwa kufanya kazi bila kujali Itikadi" amesema.
Mwisho.
Washiriki wakiwa kwenye Mafunzo.
Je, una Tangazo, Picha za Matukio, Taarifa au Habari ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi 0746057557 au 0765402289 au Email : simiyupresstz@gmail.com
إرسال تعليق